Na Jackline Martin, TimesMajira Online
BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) imezindua kampeni ya ‘Kikoba Digital’ itakayokuwa rahisi kwa watumiaji wa kikoba kuweka fedha na kukopeshana.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TCB, Adam Mihayo, alisema mapinduzi waliyoyafanya yataboresha dhana ileile inayotumika katika vikundi vilivyozoeleka vya kuweka akiba na kukopeshana.
Mapinduzi hayo ni kuwa na kikoba chenye wanachama wanaotumia mtandao mmoja wa simu na kingine kikoba mix kitakachohusisha wanachama wa mitandao tofauti.
Katika kikao kazi kinachoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kati ya Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari na taasisi za serikali, ilijitokeza hoja ya kuwa mwanachama wa kikoba kwa mitandao tofauti ya simu, jambo ambalo Mihayo aliahidi kulifanyia kazi haraka na jana amezindua kikoba kidigitali kilichokuja na suluhisho hilo.
“Tunawasogezea wateja wetu huduma hii viganjani mwao ikiwa na ufanisi zaidi na urahisi maradufu…ubunifu huu ni hatua muhimu katika sekta ya kibenki katika ulimwengu huu wa kidigitali,” alisema.
Alisema huduma hiyo inapatikana kwa urahisi zaidi kupitia simu za mkononi na benki hiyo imeshirikiana na kampuni zote za simu nchini ikiwemo Airtel, Tigo, Vodacom na Halotel ili kurahisisha namna ya kujisajili na kujiunga na kikoba mtandaoni.
“Ukiwa na kikoba mtandaoni ni salama zaidi ni rahisi kuona miamala yako na inaleta uwazi kati ya kikundi chenu cha kikoba,”alisema.
Mihayo alisema Kutakuwa na aina mbili za vikoba ambapo ni Kikoba cha kawaida na Kikoba Mix.
“Katika Kikoba Cha kawaida kwa mara ya kwanza katika historia, mteja ataweza kusajili au kujiunga na Kikoba kupitia mtandao wake wa simu kwa kupiga code fupi tu.
“ Kuhusu Kikoba Mix, Bila kuzingatia mitandao yao, Kikoba Mix inawawezesha watu kutoka mitandao tofauti kuunganika pamoja na kuunda Kikoba kwa namba zao.” Alifafanua
Mihayo alifafanua, “Kikoba ni zaidi ya fursa ya kidigitali, kwani Kikoba inabeba dhana pana ya uwazi, ujumuishi, na usalama katika uwekaji wa akiba na usimamizi bora wa kifedha. Tukitumia nyenzo hii ya teknolojia, tunaviwezesha vikundi nchini kote kusimamia mategemeo yao ya kiuchumi, kukua kiuchumi, na kujitegemea.”
Kwa upande wake, Mwalimu wa shule ya msingi na mwanachama wa kikoba Cha Good hope Tabata, Sonia Choteka alisema TCB imewasaidia kuwaletea Kikoba kiganjani kwako ambacho kitawasaidia kuhifadhi pesa kwa urahisi na kuwafanya wakina mama kuwa kitu kimoja.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi