Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Rukwa
VIONGOZI wa Dini wilayani Nkasi mkoani Rukwa wametakiwa kusimama imara na kutoruhusu kuyumbishwa na Wanasiasa katika kipindi hiki chakuelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi Mkuu mwakani.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Jumuia ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) Wilaya Nkasi Hadhiri Daruweshi akizungumza kwenye kikao cha jumuia hiyo ambapo amedai kuwa viongozi wa dini wakiyumba wanaweza kuwatoa nje ya mstari waumini wao na kubaki na sintofahamu.
Amesema kuwa wao kama viongozi wa dini jukumu lao kubwa katika kipindi hiki cha kuelekea katika chaguzi hizo kubwa ni kujikita zaidi kuhubiri amani na upendo kwa nguvu zote kwa kufanya hivyo kutasaidia kuwepo kwa amani katika taifa hili.
Hadhiri amedai kuwa kwa uzoefu katika maeneo mbalimbali duniani ambako viongozi wa dini wamechanganya siasa na dini ni lazima kuwepo kwa machafuko yanayosababishwa na kutoweka kwa amani katika jamii.
Awali Katibu wa Jumuia hiyo Mchungaji Fidelis Maheke amedai kuwa kazi ya viongozi wa dini ni kumtangaza Mungu na amani pamoja na maisha bora kwa waumini wao na kukemea vitendo vya baadhi yao viongozi wa dini kutumika na Wanasiasa
Amedai kuwa viongozi wa dini wanayo dhamana kubwa kutoka kwa watu wanaowaongoza na kuwa heshima waliyonayo wasiitumie vibaya kwa kuwachanganya Waumini wao na mambo ya kisiasa na wala wasikubali kuwa wapiga debe wa wanasiasa.
Mwinyi Abdallah Jumbe mmoja wa wajumbe wa JMAT naye amewataka viongozi wenzie kusimamia maandiko kama yalivyoandikwa kwenye vitabu vitakatifu na kuwa kwenda kinyume na maadili ni kumkosea Mungu na watu anaowaongoza.
Mmoja wa wadau wa kikao hicho Salumu Kazukamwe amewataka viongozi hao wa dini kujitahidi kusimamia maadili ya kazi kwani ni watu muhimu katika msitakhabari wa kuhakikisha amani inatamalaki nchini katika kipindi chote.
Kazukamwe ameeleza kuwa kama wanasiasa watakua na nguvu na ushawishi kwa viongozi wa dini na kutumia ushawishi wao kuwatumua taifa litakwenda pabaya bali wawe na msimamo na wajikite katika kuutangaza ufalme wa Mungu .
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu