Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Shirika la SOS Children’s Villages Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa kupinga ukatili wa kijinsia wamejenga jengo la ofisi ya Dawati la Jinsia la Wilaya ya Nyamagana ili kuweka usiri na kuimarisha utendaji kazi wa dawati hilo huku wito ukitolewa kwa jamii kuwa macho kuhakikisha ulinzi na usalama kwa watoto.
Ambapo ujenzi wa jengo hilo umegharimu kiasi cha milioni 66 huku shirika la SOS Children’s Villages Tanzania lilichangia kiasi cha milioni 55.6.
Akizungumza katika uzinduzi wa jengo la ofisi hiyo uliofanyika Mei 3,2024 kwenye kituo cha Polisi cha Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza Mratibu wa mpango wa kuimarisha familia wa shirika la SOS Children’s Villages Tanzania Mkoa wa Mwanza Elizabeth Swai, ameeleza kuwa katika ujenzi huo shirika hilo limechangia asilimia 83.7 kwa ajili ya ukamilishaji ujenzi wa jengo hilo.
Mbali na mchango huo katika ujenzi pia wamenunua vitanda vinne vya ghorofa (double darker) pamoja na magodoro manne kwa thamani ya milioni 2.4 kwa ajili ya kuwaweka waathirika wa ukatili wanapatikana usiku hivyo kufanya shirika hilo kuwa limechangia kiasi cha milioni 58.
“Tunaamini kupitia uwekezaji huu tulioweka mahali hapa watoto watapata haki zao kwa sababu masahauri yakifika hapa na kushughulikiwa na yakaenda ngazi ya kimahakama na kupatiwa haki zao watabaki salama na jamii itabaki salama kwani wataona watuhumiwa wamechukuliwa hatua stahiki,tunatoa wito kwa wadau wengine kuhakikisha jamii yetu inabaki salama kwa kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya kikatili kwenye ngazi ya mtaa,kata mpaka familia,”.
Swai ameeleza kuwa kupitia mradi wa kuzuia watoto ambao wapo kwenye hatari ya kupoteza malezi waliona kuwa kuna umuhimu wa kuhakisha kunakuwa na faragha ya waathirika wa vitendo vya ukatili wakati wakitoa taarifa za kufanyiwa vitendo hivyo pindi wanapifika kwenye madawati hayo.
Pamoja na kuhakisha masuala yanayoibuliwa kwenye jamii zile taarifa za ukatili zinazotolewa kupitia Kamati za MTAKUWWA ngazi ya mtaa mpaka Kata zinafika katika suala la kushughulikiwa.
“Masuala ya kushughulikiwa yapo kwenye Dawati la Jinsia na watoto,tuliona kabisa kwa Wilaya ya Nyamagana ofisi ya dawati ilikuwa haina usiri kulikuwa na chumba kimoja ambacho watu wanaingiliana wanashindwa kufanya mazungumzo na yule mwathirika apati usiri wa kuweza kutoa taarifa zake kwa uhuru hivyo tukaona vyema kujenga ofisi hii,”ameeleza Swai.
Sanjari na hayo ameeleza kuwa katika kuhakikisha ulinzi na usalama wa mtoto upo kwenye ngazi ya kaya hadi kwenye jamii,shirika linafanya kazi kwa ukaribu na serikali ya mtaa mpaka ngazi ya Kata na katika eneo hilo tumekuwa tukitoa elimu kwenye Kamati za MTAKUWWA ili ulinzi uimarike na watoto wawe salama.
“Tumeona matukio mengi ya kikatili yanatokea kwenye familia wanaohusika ni watu wa karibu kwa sasa hivi hatuwezi kuamini kwamba Mjomba,Shemeji amekuja tumuache na mtoto hapana ili kuhakikisha tunaweka mazingira salama kwa mtoto tusimuamini mtu yoyote kwa sababu ukatili unafanywa na mtu yoyote kwaio jamii iwe macho na sote tuwe macho kuhakikisha watoto wapo salama na kuweza kufikia malengo yao ya kimaendeleo nchini,”amesisitiza Swai.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa ameeleza uwepo wa madawati ya Jinsia na Watoto ndani ya jeshi hilo kumesaidia kuwa na ongezeko la utoajia taarifa za matukio ya ukatili hasa kwa watoto ambapo zamani matukio hayo yalikuwa hayaripotiwi kwenye vituo vya Polisi kwa sababu ya kukosa faragha na kuona aibu ni namna gani ataweza kuripoti matukio hayo katika vyumba vya mashitaka ndio wakaona ni vyema kuwa na chumba maalumu na Askari ambao wamepata mafunzo maalumu juu ya matukio hayo.
Hivyo kutokana na elimu kutolewa na uwepo wa madawati hayo matukio sasa hayafichwi na yanatolewa na hatua mbalimbali zinachukuliwa huku akitoa takwimu za matukio mbalimbali ya ukatili yaliripotiwa mwaka 2022 hadi Aprili,2024.
Mutafungwa ameeleza kuwa kwa mwaka 2022 yaliripotiwa matukio ya ubakaji 235, mwaka 2023 matukio 254, Januari hadi Aprili,2024 yameisha ripotiwa matukio ya ubakaji 48,tatizo la ubakaji bado lipo na linaendelea kuripotiwa kwa sababu watu wamepata elimu.
Matukio ya kulawiti mwaka 2022 yalikuwa 91,mwaka 2023 yalioripotiwa ni 84 na Januari hadi Aprili,2024 yaliripotiwa matukio 22, matukio ya kutupa watoto mwaka 2022 yaliripotiwa matukio 16, mwaka 2023 matukio 19 na Januari hadi Aprili mwaka huu matukio 8.
Huku matukio ya wizi wa watoto mwaka 2022 yaliripotiwa matukio 16, mwaka 2023 matukio 16 na Januari hadi Aprili mwaka huu matukio 3.
Matukio ya kuzini maalimu ni wale watu ambao wamekosa heshima na adabu na kuamua kutembea kimapenzi na ndugu zao wa karibu kama watoto,kaka kwa sababu ni kosa kisheria mtu kujihusisha kimapenzi na ndugu yake na kwa mwaka 2022 yaliripotiwa matukio 8, mwaka 2023 yaliripotiwa matukio 6 na Januari hadi Aprili mwaka huu matukio 2 yameisharipotiwa.
Matukio ya kutelekeza familia mwaka 2022 yaliripotiwa 68,mwaka 2023 matukio 48 na Januari hadi Aprili mwaka huu matukio 15 yameisharipotiwa huku ya kutorosha wanafunzi kwa mwaka 2022 matukio 31 yaliripotiwa, mwaka 2023 matukio 30 na Januari hadi Aprili mwaka huu matukio 8 yameisharipotiwa.
Pia ameeleza kuwa bado wanachangamoto ya matukio ya kuwapa mimba wanafunzi ambapo kwa mwaka 2022 matukio yalikuwa 285, mwaka 2023 yalikuwa 195 na Januari hadi Aprili mwaka huu matukio 54 yameisha ripotiwa.
Ukatili kwa watoto mwaka 2022 matukio yalikuwa 72,mwaka 2023 matukio 63 na Januari hadi Aprili mwaka huu matukio 25.
Ameeleza kuwa kwa kutambua kuwa masuala ya ukatili ni mtambuka jeshi la Polisi mkoani Mwanza hawawezi pekee yao kuzuia matukio hayo lazima washirikiane na wadau mbalimbali kupitia madawati hayo ya Jinsia na Watoto pamoja na taasisi na mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi amesisitiza kuwa kuishi bila ukatili wilayani Nyamagana na ndani ya jamii inawezekana kwa kuwa na shule na elimu inayo tembea kwa kuingia mitaa na kwenye jamii kwa ajili ya kuwaeleza umuhimu wa kutoa taarifa za vitendo vya ukatili pamoja ushirikiano wa ushahidi pindi kesi itakapofikishwa mahakamani.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â