Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar
SERIKALI imesema imepokea hoja kuhusu kubadilisha kikokotoo kwa ajili ya kuifanyia uchambuzi zaidi, maana kama ilivyosemwa kwenye risala, wafanyakazi hawaridhishwi na kanuni hizo.
“Hata hivyo, uamuzi wa kubadilisha Kikokotoo ni lazima utokane na tathmini ya kina ya kisayansi ya Watakwimu-bima. Ni matumaini ya Serikali kwamba, TUCTA itashiriki kikamilifu katika zoezi hilo na kuwasilisha maoni yatakayoimarisha zaidi mifuko.”
Hayo yamesemwa jana na Makamu wa Rais Dkt. Phili Mpango kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Mei Mosi, yaliyofanyika mkoani Arusha.
Dkt. Mpango amesema Serikali inategemea wataalam wake waishauri kuhusu suala la kikokotoo, kwani Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake wanawahakikishia wafanyakazi kwamba hakuna mtu ambaye angependa kuona watu walioitumikia nchi hii, wakiathirika kwa kukosa kiinua mgongo stahiki au pensheni zao.
“Kuhusu hoja ya kuboresha Kanuni ya ukokotoaji wa mafao, Serikali imepokea ushauri uliotolewa. Hata hivyo, ni muhimu kuzingatia kwamba uendeshaji na usimamizi wa mifuko ya hifadhi ya jamii ni suala la sayansi ya Watakwimu-bima.
Hivyo, tunawategemea wataalam wetu watushauri kuhusu suala hili la uhimilivu na uendelevu wa mifuko ya hifadhi ya jamii,” amesema Dkt. Mpango.
Amesisitiza kwamba Rais na Serikali yake wanawahakikishia wafanyakazi kwamba hakuna mtu ambaye angependa kuona watu walioitumikia nchi hii, wakiathirika kwa kukosa kiinua mgongo stahiki au pensheni zao.
“Kutokana na hali hiyo, ndiyo maana Serikali iliposhauriwa na wataalam husika, Serikali ya Awamu ya Sita ilichukua uamuzi mkubwa wa kulipa deni la mifuko ya Hifadhi ya Jamii kiasi cha sh.trilioni 2.147, hatua ambayo kwa kiasi kikubwa imeimarisha mifuko hiyo.
Vilevile, tumeendelea kuimarisha utendaji kwenye mifuko hiyo na kupunguza ucheleweshaji wa malipo ya wastaafu.”
Kuhusu hoja ya kodi kwenye mapato yasiyo ya mshahara, naomba nieleze kwamba, kodi katika mapato ya wafanyakazi inatozwa kwa mujibu wa Sheria na utaratibu wa ukokotoaji, na ukusanyaji unazingatia kanuni za msingi za utozaji kodi ikiwemo kuweka usawa kwa watu wenye kipato kinachofanana.
Amesema utaratibu huo pia unawezesha udhibiti wa vitendo vya baadhi ya waajiri wasio waaminifu, kufanya udanganyifu kwa kupunguza kiasi cha msingi cha mishahara na kuainisha kwenye mahesabu yao kiasi kikubwa cha posho na marupurupu ili kukwepa wajibu wa kulipa kodi na michango ya pensheni za wafanyakazi wao, ambazo ni haki ya msingi kwa ajili ya kuwawezesha kupata kipato cha kujikimu baada ya kustaafu.
Kama sehemu ya kaulimbiu ya mwaka huu isemavyo, “Nyongeza ya Mishahara ni Msingi wa Mafao Bora….”. Kwa wale waajiri wanaoficha mishahara katika posho, watambue kuwa licha ya kuikosesha Serikali mapato, pia wanawakosesha wafanyakazi wao mafao bora baada ya kustaafu.
Kwa muktadha huo, Serikali itaendelea kusimamia Sheria ya Kodi ili kulinda haki za wafanyakazi.
Hata hivyo alitumia fursa hiyo kutambua mchango mkubwa wa wafanyakazi katika ulipaji wa kodi.
Kimsingi, wafanyakazi ni miongoni mwa walipaji wazuri wa kodi, na mnayo kila sababu ya kujipongeza kwa mchango wenu adhimu kwa Taifa. Kupitia sherehe hizi za Mei Mosi, naomba niendelee kuyasihi makundi mengine katika jamii, kutimiza wajibu wao wa kisheria wa kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa