Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Ileje.
MKUU wa Mkoa Songwe,Daniel Chongolo, amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuimarisha ulinzi kwenye mpaka wa Tanzania na Malawi katika Wilaya ya Ileje ambao unaodaiwa kuwa na changamoto ya vipenyo vingi vinavyotumika kupitisha magendo na utoroshaji wa mbolea ya ruzuku.
Ametoa maelekezo hayo Aprili 28, 2024 baada ya kutembelea na kufanya ukaguzi katika kituo cha fodha mpaka wa Isongole, Wilayani Ileje ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya siku nne ya kukagua miradi ya maendelea, kuzungumza na watumishi ikiwemo kufanya mikutano ya hadhara.
“Lazima tukae sawa hasa kwa msimu ujao wa kilimo na tujipange kuhakikisha hakuna mbolea yeyote ya ruzuku inayovuka na kutoroshewa nchi jirani.
“Kazi ya ulinzi wa nchi ni yetu sote, hivyo kila mmoja wetu anapaswa kuwa makini kwa kila kitu kinachoingizwa hapa nchini na kutoa taarifa maana leo akifanikiwa kupitisha mbolea, kesho ataingiza silaha” aliongeza Chongolo
Aidha, Chongolo ametoa mwezi mmoja kwa Meneja wa Wakala ya barabara nchini (TANROADS)Mkoa wa Songwe, Mhandisi Suleiman Bishanga kuhakikisha anaweka bango la utambulisho wa mpaka, pamoja na ujenzi wa kibanda kwa ajili kuzuia mapato baada ya kile kilichopo kuchakaa.
Vile vile, Chongolo amemshauri Meneja wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) mkoa wa Songwe, Rashid Herth, kuhakikisha wanamaliza tatizo la ukosefu wa kizuizi cha kudumu (Road block) katika kituo hicho cha forodha Isongole.
Kadhalika, Chongolo amesema mkoa huo utapambana kuhakikisha kituo hicho cha forodha Isongole kinapandishwa hadhi kutoka daraja C hadi kufikia hadhi ya daraja B.
Kuhusu kuongezwa kwa eneo katika kituo hicho, Chongolo ameishauri TRA nchini kuona uwezekana wa kuongeza eneo hilo mapema.
Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi, alieleza kuwa shughuli za kiforodha zimezidi kuimarika katika mpaka huo baada ya serikali ya Malawi kuanza ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 36 kutoka mpakani hapo hadi makao makuu ya Wilaya ya Chitipa chini Malawi.
Hivyo,ameomba serikali kukipandisha hadhi kituo hicho cha forodha ili kiweze kujitegemea na kufanya kazi saa 24.
Awali akitoa taarifa ya utendaji katika kituo hicho, Ofisa Mfawidhi wa forodha Isongole, Charles Chacha, amesema mbali na changamoto zilizopo kituo hicho kimeendelea kukusanya mapato ya serikali kwani katika kipindi cha kufikia machi mwaka huu wamefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 126,461,596 sawa na asilimia 26.6 za malengo ya shilingi milioni 474,042,860 walizopangiwa kukusanya kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Hata hivyo, kituo hicho kimeonekana kukabiliwa na uhaba wa eneo, hivyo kuna haja kuongeza eneo kwa mapana kutokana na mahitaji maana eneo lililopo lipo jirani na ‘Bufer zone’ ambapo kuna mita 60 za hifadhi ya mto Songwe hali ambayo inaweza kuhatarisha usalama wa mizigo ya wateja kwa kuwa kumekuwa na mabadiliko ya hali ya tabia nchi.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi