November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Biteko aweka wazi utendaji wa EWURA

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,  Dodoma

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko amesema, Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeendelea kusimamia na kudhibiti shughuli za gesi asilia kwa kufanya kaguzi za mara kwa mara katika miundombinu ya uchakataji, usafirishaji na usambazaji wa gesi asilia na vituo vya kujazia gesi kwenye magari (CNG) katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es Salaam.

Akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Wizara yake Bungeni jijini Dodoma Dkt.Biteko amesema, hadi kufikia Machi 2024 jumla ya kaguzi za kawaida 25 kwenye miundombinu ya gesi asilia zilifanyika na kaguzi moja maalum ya kitaalam na kiusalama kwenye vituo vitatu vya kujazia gesi kwenye magari na karakana saba za kuongeza mfumo wa gesi asilia kwenye magari ulifanyika.

“Ukaguzi huu maalumu ulishirikisha EWURA, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB),lengo ni kuhakikisha usalama kwenye eneo la utaalam, vifaa na mazingira ya utekezaji wa shughuli zinazohusu matumizi ya gesi asilia katika magari ambapo kupitia kaguzi hizo, imebainika miundombinu na shughuli zote zinazohusisha gesi asilia hapa nchini zipo katika hali nzuri inayokidhi viwango vya ubora na usalama.”amesema Dkt.Biteko na kuongeza kuwa

“Hadi kufikia Machi 2024, EWURA ilitoa vibali sita  kwa ajili ya ujenzi  wa miundombinu ya kusambaza gesi asilia viwandani na vituo vya CNG,vibali hivyo vilitolewa kwa TPDC kwa ajili ya ujenzi wa kituo kikuu cha kuzalisha CNG kwenye eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, vituo vidogo viwili vya kupokea CNG katika kiwanda cha Kairuki kilichopo Kibaha na hospitali ya Taifa ya Muhimbili na vibali vingine viwili kwa ajili ya ujenzi wa mabomba ya kuunganisha gesi asilia kwenye kituo cha kujazia gesi kwenye magari cha Dangote na kwenye kiwanda cha kampuni ya KEDA vilivyopo Mkuranga. “

Aidha amesema , EWURA ilitoa kibali cha ujenzi kwa kampuni ya PanAfrican Energy Tanzania (PAET) kwa ajili ya ujenzi wa bomba la gesi la kuunganisha kituo cha kujazia gesi asilia kwenye magari cha kampuni ya TAQA Dalbit – Kipawa.

Kwa mujibu wa Dkt.Biteko, EWURA pia ilitoa leseni mbili za uendeshaji  kwa vituo viwili vya kujazia gesi asilia kwenye magari (CNG filling station) ambavyo  vinamilikiwa na Kampuni za TAQA Dalbit (Kipawa – Dar es Salaam) na Dangote (Mkuranga – Pwani) vinavyohudumia watumiaji wa nishati ya gesi asilia kwenye maeneo husika.

Kuhusu Shughuli za bidhaa za Mafuta ya Petroli amesema,Serikali imeendelea na usimamizi wa ubora wa vituo vya mafuta ili kuimarisha upatikanaji, usalama na ubora wa bidhaa za mafuta kwa watumiaji katika maeneo yote nchini.

Aidha amesema ,Serikali imeendelea kusimamia mazingira chanya ya uwekezaji wa ujenzi wa vituo vya mafuta vyenye ubora ambapo hadi kufikia Machi, 2024 jumla ya vituo 2,522 vilivyopo mijini na vijijini vilikidhi vigezo vya ubora na usalama na kupewa leseni ikilinganishwa na vituo 2,297 katika kipindi hicho mwaka 2022/23, sawa na ongezeo la asilimia 9.80.

Amesema ,kati ya vituo hivyo, vituo 434 vimejengwa katika maeneo ya vijijini ikilinganishwa na vituo 287 vilivyojengwa vijijini kwa kipindi hicho mwaka 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 51.22.

Dkt.Biteko amesema,katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, EWURA ilitoa leseni, vibali, kuboresha Kanuni na kusimamia ubora wa bidhaa za mafuta ambapo leseni zilitolewa kwa kampuni za mafuta kwa ajili ya kuagiza na kuuza mafuta kwa jumla.

“Leseni  30 zilitolewa kwa kampuni mpya,leseni leseni mpya nne  kwa kampuni za kuagiza na kuuza Gesi itokanayo na Petroli (LPG) kwa jumla ,pia, ilitoa leseni 27 kwa Mawakala wa Kusambaza LPG.

“ Kati ya leseni hizo, leseni 26 zilitolewa kwa Mawakala wapya ambapo serikali ilitoa leseni saba kwa kampuni zenye miundombinu binafsi ya kuhifadhi na kujaza mafuta ambapo kati ya leseni hizo, leseni sita zilitolewa kwa kampuni mpya,ilitoa leseni mpya moja ya ghala la kuhifadhia mafuta ,ilitoa leseni moja ya uwakala wa condensate”

Pia imetoa vibali vya ujenzi ) 237 ambapo vibali 233 vilikuwa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya mafuta, kimoja kwa ajili ya miundombinu ya kuhifadhia LPG, viwili kwa ajili ya matumizi binafsi na kimoja  kwa ajili ya ghala ya kuhifadhia mafuta,ilisimamia taratibu za uagizaji na usambazaji wa mafuta ili kuhakikisha upatikanaji wa mafuta ya kutosha nchini.