December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kaya 34 wilayani Rungwe hatarini kukumbwa na mmomonyoko wa udongo

Na Esther Macha, Timesmajira Online,Rungwe

KUTOKANA na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo tofauti wilayani Rungwe mkoani Mbeya Kaya 34 zipo hatarini kukubwa na mmomonyoko wa udongo huku saba tayari zikiwa zimeathiriwa ,hivyo kutakiwa kuhama maeneo hayo ili kuepuka athari ambazo zinaweza kujitokeza.

Kauli hiyo imetolewa Aprili 19 ,2024 wakati Mkuu wa Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya Jaffar Haniu alipoambatana na Kamati ya Maafa Wilaya kutembelea na kujionea athari zinazoendelea kujitokeza kufuatia kukatika kwa mawasiliano ya barabara ya Kapugi-Lyenje kupitia mto Kiwira.

Haniu akiwa na kamati ya ulinzi na usalama wilaya ameweza kukagua makazi ya wananchi wa kijiji cha Lyenje yaliyoathiriwa na mvua hizo pia kutembelea maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kambi ya muda ya wananchi walioathiriwa .

“Mvua hizi zinazoendelea kunyesha karibu nchi nzima na zinaendelea kuleta athari hivyo kusababisha ardhi kuleta mmeng’enyo ambao umechangia barabara muhimu kwa uchumi wa Rungwe kukatika, “amesema Haniu.

Hata hivyo Haniu amezitaka kaya saba ambazo watu wake wanaotakiwa kuhama wahame mara moja na kujihifadhi katika eneo maalumu lililotengwa katika kijiji cha Lyenje.

Aidha amesema barabara iliyoathiriwa ni kiungo muhimu cha usafirishaji wa mazao ya kahawa, ndizi, parachichi na mahindi kutoka upande mmoja kwenda mwingine huku mashamba mbalimbali kuathiriwa.

Bonde la mto kiwira ni maarufu kwa kilimo cha kahawa,migomba na mahindi lakini kwa hatua hii wakulima wametahadharishwa kuendelea kuwa makini ili kujiepusha na maafa yanayoweza kujitokeza.

Mmomonyoko wa udongo umekata barabara na miamba yake kufukia mto Kiwira ambao humwaga maji yake Ziwa Nyasa.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya ameeleza kuwa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) kuendelea kufanya utafiti wa namna bora ya kurejesha mawasiliano ili wananchi waendelee kunufaika na matunda ya nchi yao.