December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TBS yaanika mafanikio miaka mitatu ya Samia

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeanika mafanikio makubwa ambayo shirika hilo limepata kwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, pamoja na hatua mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa kwa ajili ya kuwezesha biashara ndani na nchi ya nchi.

Mafanikio hayo yameanikwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Yusuf Ngenya, wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini katika mkutano ulioandaliwa na ofisi ya Msajili wa Hazina.

Alisema shirika limefanikiwa kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia ofisi za kanda saba ambazo ni Kanda ya Kaskazini (Arusha) ,Kanda ya Kusini (Mtwara) ,Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya).

Nyingine ni Kanda ya Magharibi (Kigoma) ,Kanda ya ziwa (Mwanza) ,Kanda ya Kati (Dodoma) na Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam).
Kanda hizi zina ofisi katika mipaka, bandari pamoja na viwanja vya ndege.

Aidha, Dkt. Ngenya amesema Shirika limewekeza kwenye ununuzi wa vifaa vya maabara vya kisasa kwa kutumia fedha za ndani pamoja na misaada kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo.

Kwa upande wa ithibati za umahiri katika maabara, Dkt. Ngenya alisema Shirika lina maabara 12 zilizopo Ubungo Dar es Salaam, ambapo zimehakikiwa na kupatiwa cheti cha ithibati ya umahiri wa kimataifa (accreditation).

“Hatua hiyo inapelekea majibu ya sampuli kutoka katika maabara hizo kuaminika kokote duniani na hivyo kurahisisha biashara,” alisema Dkt. Ngenya.

Kuhusu utoaji huduma kupitia mifumo ya kielektroniki, alisema
Shirika limetengeneza mifumo ya kielektroniki inayotumika kutoa huduma zake.

“Uanzishwaji wa mifumo ya kielektroniki imewezesha wateja kupata huduma za TBS popote walipo kwa wepesi na haraka hivyo kupunguza gharama kwa wateja,” alifafanua Dkt. Ngenya.

Aidha, amesema imeweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wazalishaji.

Kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya viwango 1,721 vya kitaifa viliandaliwa sawa na asilimia 101.2 ya lengo la kuandaa viwango 1,700.

Kwa mujibu wa Dkt. Ngenya viwango hivyo viliandaliwa katika nyanja mbalimbali. Pia alisema TBS imeshiriki katika uandaaji wa viwango vya kibiashara vya Afrika Mashariki na Afrika nzima.

Aliongeza kwamba Serikali kwa kupitia TBS imekuwa ikitenga zaidi ya milioni 250 kwa dhumuni la kuhudumia wajasiriamali wadogo bila ya malipo yoyote.

“Kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya leseni za ubora wa bidhaa 2,106 zilitolewa kwa wazalishaji mbalimbali wa bidhaa hapa nchini sawa na asilimia 105.3 ya lengo la kutoa leseni 2,000. Kati ya leseni hizo, jumla ya leseni 1,051 zilitolewa bure na kwa Wajasiriamali wadogo,”alisema.

Aidha, alisema kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya wadau 5,789 kutoka mikoa mbalimbali nchini walipewa mafunzo hayo.

“TBS imeendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo (MSEs) na wazalishaji ili kuwawezesha kuzalisha bidhaa zinazokidhi matakwa ya viwango vya ubora na usalama na hatimaye kukidhi ushindani wa masoko ya ndani, kikanda na kimataifa,” alisema.

Aliongeza kwamba Shirika limeandaa utaratibu wa kukagua viwanda vyote hapa nchini ili kuhakikisha kwamba vinazalisha bidhaa zenye ubora unaotakiwa.

Alifafanua kwamba kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya leseni za ubora wa bidhaa 2,106 zilitolewa kwa wazalishaji mbalimbali wa bidhaa hapa nchini sawa na asilimia 105.3 ya lengo la kutoa leseni 2,000.

Kuhusu ukaguzi wa bidhaa zinazotoka nje ya nchi, Dkt. Ngenya, alisema TBS hudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka nje kwa kutumia mfumo wa Pre-Shipment Verification of Conformity to Standards (PVoC) pamoja na kufanya ukaguzi pindi bidhaa zinapowasili nchini (Destination Inspection).

Kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya shehena 100,851 kabla hazijaingizwa nchini sawa na asilimia 99 ya lengo la kukagua shehena 102,083. Pia, jumla ya bidhaa 151,570 kutoka nje ya nchi zilikaguliwa baada ya kufika nchini sawa na asilimia 77 ya lengo la kukagua bidhaa 197,417.

Alisema TBS hudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka nje kwa kutumia mfumo wa Pre-Shipment Verification of Conformity to Standards (PVoC) pamoja na kufanya ukaguzi pindi bidhaa zinapowasili nchini (Destination Inspection).

Alisema kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya shehena 100,851 zimekaguliwa kabla hazijaingizwa nchini sawa na asilimia 99 ya lengo la kukagua shehena 102,083.

Pia, alisema jumla ya bidhaa 151,570 kutoka nje ya nchi zilikaguliwa baada ya kufika nchini sawa na asilimia 77 ya lengo la kukagua bidhaa 197,417.