November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bomba la Mafuta Chongoleani wapata maji ya uhakika

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Tanga

Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira Tanga (Tanga UWASA) inatekeleza mradi wa kuboresha miundombinu inayolenga kuimarisha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi katika maeneo ya Kata za Mabokweni, Mzizima na Chongoleani zenye mitaa kumi na wakazi wapatao 26,071.

Mbali na kuboresha hali ya huduma kwa wakazi wa maeneo hayo lakini pia kwa watumiaji wengine kama viwanda, biashara pamoja na kambi ya kampuni inayohusika na ulazaji wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mnzava akifungua maji kuashiria upatikanaji wa maji ya uhakika kwenye kambi ya Bomba la Mafuta Chongoleani jijini Tanga

Hayo yamesemwa Aprili 14, 2024 na Mhandisi wa Tanga- UWASA Violeth Kazumba mbele ya Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava, mara baada ya Mwenge wa Uhuru kutembelea mradi wa kuboresha hali ya upatikanaji wa maji Chongoleani.

Akisoma taarifa hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga- UWASA, Mhandisi Geofrey Hilly, Mhandisi Kazumba amesema utekelezaji wa mradi huo ulianza Novemba 2022 ambapo ujenzi wake umefanywa na Mkandarasi M/S Engineering Plus wa Dar es Salaam na umekamilika Machi 30, 2024 kwa asilimia 100.

Hadi sasa mradi unatoa huduma kwa jamii, na Mamlaka ya Maji inaendelea kufanya maunganisho ya maji kwenye matawi pamoja na watu binafsi kwa mujibu wa maombi yanayopokelewa kutoka kwa wahitaji.

Zoezi la uhakiki wa nyaraka kwenye mradi wa uboreshaji maji Kambi ya Bomba la Mafuta Chongoleani huku baadhi ya wanaoshuhudia ni Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maji Sophia Swai (kushoto) na Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo (wa pili kushoto).

Aidha ujenzi wa mradi huu ulihusisha ununuzi na ulazaji wa mabomba (kipenyo cha 315 mm, 250mm, 200mm, 150mm na 110mm) kwa urefu wa mita 24,000, ununuzi na ufungaji wa viungio vya mabomba pamoja na ujenzi wa chemba 54 na usimikaji wa alama 309 za kuonesha njia ya mabomba.

“Mradi huu umefadhiliwa na taasisi inayohusika na ulazaji wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani Tanzania, ambapo usanifu wake umekadiriwa kugharimu sh. 2,352,201,500 na hadi sasa Mkandarasi ameshalipwa sh. 1,823,766,540 sawa na asilimia 79.46,” amesema Mhandisi Kazumba.

Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maji Sophia Swai (kushoto), na Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Upendo Lugongo (kulia) wakifurahia kutoka kwa maji Kambi ya Bomba la Mafuta Chongoleani

Mhandisi Kazumba amesema faida kuu za mradi huo ni kuwezesha wakazi wa Kata za Mzizima, Mabokweni na Chongoleani wapatao 26,071 kupata huduma ya maji safi kila siku kwa saa 24.

Lakini huduma hiyo itawezesha uwekezaji zaidi katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na wawekezaji wa Bomba la Mafuta Ghafi (EACOP).

Kwa upande wake Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2024 Godfrey Mnzava ameridhishwa na mradi huo hasa kwenye kutangaza zabuni kupitia mfumo, kwani kwa njia hiyo watapata kampuni ama wakandarasi wenye uwezo na wale wababaishaji mfumo utawaondoa kama sio kuwakataa.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mnzava akioneshwa michoro ya mradi wa uboreshaji maji, na Mhandisi Violeth Kazumba wa Tanga- UWASA