Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
MKURUGENZI wa kampuni ya My Fish Tanzania, Elpidius Mpanju amesema
upatikanaji wa chakula cha samaki nchini na ukosefu wa mitaji ni changamoto
inayowakabili wafugaji wa samaki kwa njia ya vizimba
Mpanju ameeleza changamoto hizo Aprili 8,2024 wakati wa Kongamano la Uchumi wa Buluu na maonesho ya picha yaliondaliwa na Chama cha waandishi wa habari za kuendeleza shughuli za bahari na uvuvi Tanzania(TMFD),lililofanya jijini
Mwanza.
Amesema serikali imekuwa ikihamasisha ufugaji wa samaki lakini upatikanaji wa chakula cha samaki ni tatizo huku mahitaji yakiwa ni makubwa,sekta binafsi na watu wenye uwezo wawekeze na kujenga viwanda vya kukizalisha nchini baada ya kuagiza nje kwa fedha za kigeni kwani kikizalishwa ndani kitanunuliwa kwa bei nzuri.
Pia,wafugaji hao wa samaki wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu
wa mitaji kutoka taasisi za fedha hivyo wanahitaji kupata mikopo wazalishe
kwa tija na kushindana katika soko.
“Tuna tatizo la mitaji kutokana na taasisi za fedha kwa sababu haziuamini
uwekezaji wa viumbe maji licha ya kuwa vyanzo na soko lipo la uhakika,hatutaki
kukimbia miradi yetu,tunachohitaji watusaidie mikopo tuweze kukua,”amesema.
Mkurugenzi huyo wa My Fish Tanzania ametaja changamoto nyingine ni mabadiliko
ya hali ya hewa pia wamevamiwa na magugu maji ambayo hupunguza hewa ya
Oksijeni ambayo yamesababisha washindwe kuwalisha samaki chakula.
Aidha amesema mabadiliko ya teknolojia yamesababisha wafugaji wa
samaki wasio na uwezo kutozalisha kwa tija kwa sababu mabomba ya vizimba vya
chuma wanavyofugia kuoza na kuvunjika,alishauri watumie vizimba vilivyotengenezwa
kwa mabomba ya plastiki ambayo ni rahisi kufugia samaki.
Mpanju amewashauri vijana walio wengi waliokosa ajira ama walioajiriwa na
kupata maslahi madogo ili kuondoka na kadhia hiyo, njia sahihi ni kuchangamkia uchumi wa buluu baada ya serikali kubadilisha sera na sheria ya uvuvi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Said Mtanda,kutokana na
changamoto ya mikopo amesema atazungumza na Benki ya Kilimo (TADB),vijana wakopeshwe
mikopo nafuu wanufaike kwa rasilimali zinazotokana na uchumi wa buluu.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa