Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
WAUMINI wa Dini ya Kiislamu wamehimizwa kuishi kwa upendo,umoja,kudumisha amani ya nchi pamoja na kutoa zaka huku wakimwombea Rais Dk.Samia Suluhu Hassan na nchi kwa ujumla.
Pia wamehimizwa wakaboreshe taarifa zao katika daftari la kudumu la wapiga kura ili wawe na sifa yakupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Wito huo umetolewa Aprili 10,2024 na Sheikh wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Hassan Kabeke wakati akitoa hotuba ya sala ya Eid El Fitri kwa waumini hao iliofanyika kimkoa katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
Amesema mwezi Mtukufu wa Ramadhani umewaunganisha na kuwaweka pamoja Waislamu wote hivyo wajitahidi kuungana na kuwa wamoja bila kujali itikadi zao za kidini katika kudumisha amani,upendo na mshikamano.
“Hatuwezi kupata maendeleo tukiwa tumegawanyika na haifai baada ya Ramadhani turudi kunyoosheana vidole huyu Shia, Ibadhi au Suni,haitusaidii,tusimame pamoja na tuwaheshimu viongozi wetu na Mwenyezi Mungu hawezi kutuacha,”amesema Sheikh Kabeke.
Amewaasa Waislamu wa Mwanza wawe wamoja wasiwe watu wa kutukana ama kwenda kumpiga mwislamu mwenzao kwa kuwa huo ni ukafiri kwa sababu Uislamu ni dini ya amani,hivyo waendelee kumcha Mungu na kutenda mema muda wote.
“Dini yenu ni ya amani,unapokutana na mtu unamtamkia amani (Salaam Aleykum)pia imetuwekea utaratibu wa kukumbuka kutunza amani na Tanzania inasifika kwa hilo.Itakuwa ajabu mwislamu kuvunja amani ambayo hata ndani ya familia tunaitaka na kuna umuhimu wa kuitunza,”amesema Sheikh Kabeke.
Amewasistiza kuishi kwa usalama na jamii mitaani bila kubughudhiana kwa sababu dini yao ni ya amani,asitokee mwislamu akaivunja amani au kutoa lugha na maneno yanayoweza kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani.
Akizungumzia zaka amesema,wapo waislamu ni matajiri lakini hawatoi fungu la kumi la mapato yao (zaka) na kuwataka kutimiza takwa hilo na kuongeza kuwa majanga yanayotupata yanasababishwa na kutokutoa zaka.
“Zaka haitolewi kwa kujisikia kuwa leo nina elfu 10,nampa masikini la! Ni fungu la kumi la mapato yako na wengine ni wakulima hawatoi zaka ya mazao,pia wachimba madini na wafugaji, tulipeni zaka ni wajibu tumeusahau,”amesema Sheikh Kabeke.
Pia ameeleza watu wengi wanakumbwa na matatizo kwa sababu ya kutokutosheka,hivyo tajiri mkubwa ni aliyetosheka katika nafsi yake na kuwataka waislamu waridhike na walichojaliwa,waishi kwa hofu na kumwogopa Mwenyezi Mungu.
Pia waiishi Q’uran kwa kula,kulala,kufanya na kuacha yote yaliyokatazwa na Mwenyezi Mungu huku wakijiandaa kabla ya kuondoka duniani kwani, siku hiyo ikifika hakuna ujanja.
“Mungu hafanyi jambo bila sababu,mtalipwa kwa matendo mliyotenda kwani yeye asema mmefaradhiwa funga.Hivyo usidhani wewe ni wa kwanza,kumbukeni kumcha Mungu maana yake asikukute alipokukataza akukute alipokuagiza,”amesema.
Sheikh huyo wa Mkoa wa Mwanza amewasistiza waislamu kuzingatia mafundisho ya Mwenyezi Mungu,waendelee kumcha na kutenda mema huku akiwaonya wanaotumia vileo na dawa za kulevya aina ya mirungi kuwa imeharamishwa na imewaharibu vijana wengi.
“Ramadhani ilitutengeneza tukaswali tukaacha ulevi tukaacha kutukana leo ni siku ya kusaidia yatima waliokosa wazazi wao,wajane na masikini,tuwatafute yatima tuwasaidie.Tujiulize hivi baada ya Ramadhani tutakuwa watu wa namna gani? ” amesema kwa kuhoji.
Kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, mwaka huu,Sheikh Kabeke amewataka waislamu kwenda kuboresha taarifa zao katika daftari za wapiga kura wapate sifa ya kupiga kura.
” Ni mwaka wa uchaguzi wa serikali za mitaa, tuhakikishe amani inadumu,tukahuishe taarifa zetu tuwe na uhalali wakupiga kura,unayetaka uongozi nenda chama chochote uchukue fomu ya kuomba kugombea,siku ya kupiga kura tusibaki nyuma tujitokeze kuchagua viongozi tunaowataka,” amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akitoa salamu amewatakia kheri waislamu na Watanzania katika kusherehekea Eid El Fitri kwa amani huku akitumia fursa hiyo kuwaomba ushirikiano na kumwombea katika kutekeleza majukumu yake.
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza,Wakili Kiomoni Kibamba amesema funga ni moja ya ibada ya Mwenyezi Mungu,hivyo baada ya Ramadhani waislamu na wananchi wote wa Jiji waendelee kudumisha amani,upendo na kusherehekea kwa utulivu na amani.
Mkurugenzi wa Shirika la Kivulini,Yasin Alli amesema uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika nchini usiwe chanzo cha kuvunja amani.
“Tanzania imepita katika chaguzi nyingi licha ya tofauti za itikadi za dini na vyama tukubaliane na kutofautiana kwa hoja,tusivuruge amani na kutomcha Mungu,tuzingatie yote yaliyokatawaza.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa