November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC. Mpogolo: Ilala hatuna deni kwa Rais Samia

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online,Dar

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema,wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala na wananchi wa Ilala hawana deni kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika upande wa maendeleo.

Mkuu wa Wilaya huyo amesema hayo Aprili 6, 2024 katika mafunzo ya siku moja yaliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Shirika la Reli Tanzania (TRC) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa wajumbe 900 wa CCM Jimbo la Ilala yalifanyika jijini Dar es Salaam ambayo yaliofunguliwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Side.

Mpogolo amesema, mafanikio na kazi zilizofanywa na Rais Samia nchini kwa sasa deni lililopo kwa wananchi hususani wakazi wa Ilala ni kumshukuru kwa kumuunga mkono kumpa kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi Mkuu.

“Kwa aliyofanya Rais wetu amefanya mengi ikiwa ni pamoja na kutupatia fedha za kutosha ambazo zimeelekezwa katika miradi ya maendeleo na Wilaya ya Ilala, hakuna sehemu ambayo tumekosa miradi katika majimbo ya Ilala, Segerea na Ukonga,”.

Aidha ametumia nafasi hiyo, kuwataka wananchi wa Wilaya hiyo,kujitokeza kwa wingi kujiandikiaha katika daftari la Kudumu la kupiga kura pamoja na kupiga kura bila hofu huku akiwahakikishia ulinzi na usalama wa kutosha wakati wote.