Prof.Ole Gabriel:Idadi Majaji wa Rufani imeongezeka zaidi ya asilimia 100
Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
WAKATI Tanzania ikiadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kumekuwepo na ongezeko la Majaji wa Rufani kutoka Majaji wa Rufani 16 hadi kufikia 03 Septemba 2023 idadi ya Majaji wa Rufani imeongezeka na kufikia 35 ikiwa ni zaidi asilimia 100.
Ongezeko la Majaji wa Mahakama ya Rufani limeenda sambamba na uanzishwaji wa Masjala ndogo ya Mahakama ya Rufani nchini.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Aprili 5,2024 na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,Prof.Elisante Ole Gabriel wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika miaka 60 ya Muungano.
Prof.Elisante amesema kuwa wakati Dkt. Samia Suluhu Hassan akiingia madarakani Machi 2021 kulikuwa na Majaji wa Rufani 16 na katika uongozi wake hadi kufikia 03 Septemba 2023 idadi ya Majaji wa Rufani imeongezeka na kufikia 35 ikiwa ni zaidi asilimia 100.
“Ongezeko la Majaji wa Mahakama ya Rufani kwa sasa linawezesha majopo 11 ya majaji watatu, majopo saba ya Majaji watano na majopo Matano ya Majaji saba kuendesha vikao vya Mahakama ya Rufani kwa wakati mmoja.
“Idadi ya Vituo vya kusikilizia mashauri ya Mahakama ya Rufani imeongezeka na kutoka 16 wakati wa Mhe. Dkt. Samia akiingia madarakani na kufikia vituo 18 mpaka sasa.
“Vituo vya usikilizaji wa Mashauri ya Mahakama ya Rufani viko katika Masjala za Mahakama Kuu za Arusha, Dar es Salaam, Bukoba, Dodoma, Iringa, Kigoma, Mbeya, Morogoro, Moshi, Musoma, Mtwara, Mwanza, Shinyanga, Songea, Sumbawanga, Tabora, Tanga na Zanzibar.
Aidha ametaja faida zilizotokana na kuongezeka kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani ikiwa ni pamoja na kupunguza mrundikano wa mashauri, kusogeza huduma karibu zaidi na Wananchi katika Masjala zote za Mahakama Kuu, Mashauri kusajiliwa na kuamuriwa kwa wakati na kupungua mzigo kwa majopo yaliyokuwepo.
Pia amesema ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Pemba, ambao utaanza hivi karibuni ni miongoni mwa mafanikio yanayolenga kusongeza huduma za utopaji haki karibu na wananchi. Uwepo wa Kituo hicho utaiwezesha Mahakama ya Rufani kuwa na Masjala yake ndogo, hivyo kuongeza idadi ya Vikao vya Mahakama kwa upande wa Zanzibar.
Pamoja na hayo ameeleza Historia ya Mahakama ya Rufani ambapo Mwaka 1963 mfumo mpya ulianzishwa ambao uliunganisha Mahakama za wenyeji na Mahakama Kuu na kuondoa ubaguzi wa rangi na ukatenganisha Mahakama (judiciary) na Utawala (Executive) ambapo Sheria za kimila zilitambuliwa na kuunganishwa ili kuondoa migongano ya sheria (Conflict of laws). Mabadiliko ya mwaka 1963 yaliweka msingi wa mfumo wa Mahakama zilizo chini ya Mahakama Kuu ambao upo hadi sasa.
“Katika kipindi hicho rufaa kutoa Mahakama Kuu zilipekwa Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki (E.A.C.A) na Jaji Mkuu wa kwanza Mtanzania aliyeongoza Mahakama Kuu ya Tanzania alikuwa Mhe. Augustino Saidi ambaye alihudumu kuanzia mwaka 1971 mpaka mwaka 1977,”amesema.
Amesema Rufaa za kutoka Mahakama Kuu ziliendelea kupelekwa Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki hadi mwaka 1979 ilipoanzishwa Mahakama ya Rufani ya Tanzania ikianza na Majaji wa Rufani watano (5), idadi hiyo ikimjumuisha Jaji Mkuu, wakifanya kazi katika Masjala ya Dar es Salaam.
More Stories
TAKUKURU,rafiki yanufaisha wananchi Mwanza
Mhandisi Samamba awasisitiza maafisa madini kusimamia usalama wa migoni msimu wa mvua
Wapinzani kutimkia CCM ishara ya ushindi Uchaguzi Serikali za Mitaa