November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maboresho hospitali ya Wilaya yapunguza vifo vya wanawake na watoto

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Kalambo

Hospitali ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa katika kipindi cha miezi sita imewezesha wanawake 860 kujifungua kati yao 741wakijifungua kwa njia ya kawaida na 119 kwa njia ya upasuaji huku vifo vya mama na mtoto vikipungua kutoka 11 hadi 8 kwa mwaka 2023.

Hosptali hiyo inahudumia wanawake wanaojifungua wapatao 8-9 kwa siku mpaka Machi 2024 jumla ya wanawake 2218 wamepatiwa huduma za mama na mtoto huku kila mwezi wanawake 164 wamekuwa wakihudhuria huduma hizo .

Hayo yamebainishwa na Mratibu wa Huduma za Mama na Mtoto wilayani humo Bakari Ndarusi wakati wa utoaji elimu kwa wanawake wanao jifungua,ambapo amesema hospitali hiyo inahudumia wastani wa watoto 180 hadi 200 na watoto njiti 6 kila mwezi.

Kwa upande Muuguzi Mkuu wa hosptali hiyo , Diana Didi amesema licha ya hilo hospitali hiyo imekuwa ikihudumia wanawake 30 kwa siku na kuwataka wanawake kujenga mazoea ya kuwahi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya pindi wanapopatwa na uchungu wa kujifungua ili kuokoa vifo vya mama na mtoto.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Sunday Wambura amebainisha kuwa halmashauri imepokea fedha million mia nne kwa ajili ya umaliziaji wa zahanati 8 na smillion mia tatu kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vituo vipya vya afya.