November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Azam TV yazindua filamu mpya

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

KATIKA kuhakikisha wapenzi wa Filamu wanaelimika na kuburdika chaneli ya Sinema zetu, kupitia kisimbuzi cha Azam Tv, imezindua tamthilia mpya inayoitwa ‘Bunji’.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jijini Dar es salaam, Msimamizi Mkuu wa Kituo cha Sinema Zetu, Sophia Mgaza alisema wanaendelea kuisukuma sanaa kimataifa ukanda wote hasa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara

Alisema, tamthiliya hiyo itaonyeshwa kwa mara ya kwanza Aprili Mosi mwaka huu, katika chaneli namba 103 ya sinema zetu kuanzia jumatatu mpaka alhamisi saa 1 na nusu hadi saa 2 kamili

Aidh, Mgaza alisema tamthilia ya ‘Bunji’ inamuhusisha kijana mmoja ambaye ni mhitimu wa Udaktari na ni Daktari bingwa wa magonjwa ya uzazi, lakini ndoto yake ni kuwa mpiganaji wa kulipwa.

Akiendelea kuelezea Tamthilia hiyo, Mgaza alisema baada ya kuhitimu, analazimika kufanya kazi katika hospitali ya familia na siku ya kwanza anagundua kuwa familia yake inafanya biashara haramu kupitia mgongo wa hospitali.

“Hali hii inamfanya Banju kuishuku familia yake kuhusika na kifo Cha mama yake, katika kutafuta ukweli, anaisababishia familia yake balaa kubwa, kitendo kinachosababisha kaka yake Ayubu kupigwa risasi na baba yake mzazi huku Banji akitoroka kuelekea Mbeya ambako anaamini ataupata ukweli kuhusu kifo Cha mama na familia yake ambayo hakuwahi kukutana nayo” Alieleza Mgaza.

Mgaza alisema, Tamthiliya hiyo imesheheni wasanii nguli na wale wanaochipukia ambayo pia imeandaliwa na Jitu la Msituni Film.

“Miongoni mwa waigizaji mashuhuri katika tamthiliya hii ni pamoja na Isarito Mwakalindile, Twaha Kiduku, Nyota Waziri, Dkt. Nnyaka Godwin, Carpoza Edward, Fatma Hassan n.k”

Mmoja wa waigizaji wa tamthiliya hiyo, Isarito Mwakalindile aliishukuru timu yake yote iliyohakikisha tamthiliya inafika mbali na changamoto walizokutana nazo wakati wakiandaa, timu hiyo ilihakikisha tamthiliya inakamilika kwa wakati na kwa viwango vya juu.