December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

AQRB yakabidhi zawadi kwa shule washindi shindano la Insha 2022/23

Na Rose Itono, timesmajira

BODI ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi ( AQRB) imemkabidhi Mkuu wa Shule ya Sekondari Usagala iliyopo Mkoani Tanga zawadi ya fedha taslim Sh.500,000 baada ya mwanafunzi wake Nurdin Fiomi kuibuka mshindi wa kwanza Kitaifa kwenye mashindano ya uandishi wa Insha yaliyoandaliwa na bodj hiyo kwa mwaka 2022/23

Pia imekabidhi kiasi cha Sh 100,000 kwa mwanafunzi huyo baada ya kushika nafasi ya kwanza Mkoa na kufanya mwanafunzi huyo kujishindia kiasi cha Sh.600,000

Akizungumza mara baada ya kukabidhi zawadi hiyo mwishoni mwa wiki Ofisa Habari wa AQRB Hamisi Sungura alisema pia shule hiyo imejishindia zawadi ya Sh. 300,000 kama motisha ya kuwezesha shule zingine nchini kuona umuhimu wa kuwashawishi wanafunzi wao kushiriki mashindano kila yanapotangazwa

Sungura amesema lengo la mashindano hayo ni kuwahamasisha wanafunzi kuzijua taaluma za Ubunifu Majengo na Ukadiriaji Majenzi

Amesema wanafunzi wengi wamekuwa wakizichanganya taaluma hizi na ile ya Uhandisi hivyo kutokana na hali hiyo AQRB imekuwa na programu mbalimbali zinazohusisha utoaji wa elimu juu ya taaluma hizi ikiwa ni pamoja na kuandaa mashindano ya uandishi wa insha kisha kutoa zawadi kwa washindi waliofanya vizuri

” Kwa kipindi cha mwaka 2022/23 tulipokea zaidi ya insha 500 kutoka shule mbalimbali zilizopo Tanzania Bara ikiwepo shule ya Sekondari Usagala na Tanga Ufundi na kupata washindi wa Kitaifa na Mkoa ambao Leo tunawapatia zawadi zao kupitia Wakuu wa shule hizo ili wawafikishie wanafunzi wao,” alisema Sungura na kuongeza kuwa wameamua kupitishia kwa Wakuu wa Shule ili iwe rahisi kuwapata wanafunzi wao kwani wengine tayari wamemaliza shule.

Amesema awali program hii ya kutembelea mashuleni ilikuwa ikizihusisha shule za Sekondari na vyuo lakini kutokana na serikali kuanzisha mtaala mpya wa amali progranu hii itazihusisha pia shule za msingi ili wakue wakizifahamu taaluma hizo

Kwa upande wake Ofisa Udhibiti wa AQRB ambaye ni Mkadiriaji Majenzi Angel Michase amesema zawadi zinazotolewa kwenye mashindano ya uandishi wa insha ni kama motisha ya kuwavutia wanafunzi wengi kupenda kusomea taaluma hizi ambazo zinaendana na mtaala mpya wa amali ulioanzishwa maalumu na serikali mwaka 2024 ili kuwajenga wanafunzi wanapomaliza masomo yao waweze kujiajiri

“Nawashauri wanafunzi msome masomo ya sayansi ili naadaye mjiunge na vyuo vya elimu ya juu katika masomo ya Ubunifu Majengo na Ukadiriaji Majenzi taaluma ambaxo zinahusika moja kwamoja na sekta ya ujenzi na ni rahisi sana kujiajiri,’amesema Michase

Aidha ameipongeza shule ya Sekondari Usagala kuibuka mshindi wa kwanza Kitaifa na ile ya Tanga Ufunndi kwa kutoa mshindi na kupata zawadi kwenye mashindano hayo

Naye Mkuu wa shule ya Sekondari Usagala Mwalimu Alex Birumo ameipongeza AQRB kwa kuona umuhimu wa kuandaa mashindano hayo na kuahidi kuendelea kushawishi wanafunzi wake wengi zaidi kwenye mashindano yajayo

Hata hivyo Mkuu wa shule ya Tanga Ufundi Mackmaster Luzilo ameshukuru pia AQRB kukabifhi zawadi za ushindi kwa mwanafunzi wao na shule na kuahidi kuendelea kuhamasisha wanafunzi wake wengi zaidi kushiriki