Na Mwandishi wetu, timesmajira
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amefanya ziara maalum ya kuwafariji wananchi wa maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kusini Pemba huku akitoa sadaka ya futari kwa wananchi hao.
Ziara hiyo ambayo ilianza mapema wiki hii Kisiwani Unguja, ni Muendelezo wa Mila, Silka na Ada ya Mtangulizi wake Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, ya kila Mwaka, inayolenga pia kuwafikia watu, hasa ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Akitoa nasaha zake kwa Wananchi ziarani humo Othman, amesema kutembeleana na kujuliana hali kunaleta Umoja na mapenzi hasa ndani ya mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan, ambapo yapo Mafunzo mengi Mema ambayo tunapaswa kudumu nayo, huku akiwataka Viongozi wa Chama wa ngazi ya Mkoa kuendeleza utaratibu huo kwawale ambao hawakupata fursa ya kufikiwa.
“Tukiendelea na Silka hizi ndani ya mwezi huu hakika zitaijenga athari njema katika nyoyo zetu hata baada ya mwezi kuisha”.
Othman ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha ACT Wazalendo akiambatana na Mke wake Mama Zainab Kombo Shaib, yupo kisiwani Pemba kwa ziara hio maalum ya siku tatu.
Pamoja na kuwatakia waumini, ramadhani njema yenye Amani, Kheri na Baraka, Othman ametoa sadaka ya futari kwa wananchi hao ambao wanachangamoto mbalimbali.
Naye, Mzee Haji Shaib Hamad (95) wa Pujini Chambani, ameeleza faraja wanayoipata wananchi kwa kufikiwa na kiongozi huyo akisema; “Kwahakika Wananchi tunafarijika kufikiwa kwetu nawe, kwani tuna mengi ambayo tunahitaji kuyaeleza kwenu, na hakika ya kiongozi bora ni mwenye kuwafikia na kuwaskiliza wananchi wake”. Amesisitiza Mzee Haji akiupongeza mwenendo huu endelevu na mwema aliouasisi Maalim Seif.
Katika Ziara yake hiyo, Othman amewatembelea na kuwajulia-hali, Wagonjwa na Wazee mbali mbali wasiojiweza, na pia kuwapa Mkono wa Pole Wafiwa, wakiwemo wa Majimbo ya Chambani, Kiwani, Mtambile, Mkoani, Wawi, Chake chake na Chonga ya Wilaya za Chake na Mkoani, ndani ya Mkoa wa Kusini Pemba.
Wananchi ambao Othman amewatembelea ni pamoja na Mtumwa Rashid Faki, Haji Shaib Hamad, Zuhura Shehe Mohamed, Dukani Khamis Salim, Ali Amir Juma, Kombo Hamad Hamad na Salama Rashid Ali.
Viongozi na Watendaji wa ngazi mbali mbali za Chama, wameambatana na Othman katika Ziara hiyo, wakiongozwa na Mratibu wa Chama Kisiwani Pemba, Said Ali Mbarouk.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua