Na Mwandishi wetu,Dodoma
MKURUGENZI Msaidizi Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bi. Jane Kikunya amesema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wadau mbalimbali katika masuala ya uratibu wa maafa nchini ili kuendelea kuwa na stahimilivu na maafa.
Ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifungua Warsha ya siku moja iliyowakutanisha wadau kutoka Serikalini, Makampuni ya simu, Taasisi zinazotoa Misaada ya kibinadamu kwa lengo la kujadili fursa na kutoa maoni kuhusu njia sahihi ya ujumuishaji wa teknolojia ya simu katika mifumo ya kutoa tahadhari ya Awali .
Warsha hiyo ilihudhuriwa na wataalam kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Mifugo, Wizara ya Maji, Wizara ya Afya, Wizara ya Kilimo pamoja na Taasisi ikiwemo TCRA, TMA, REDCROSS, makampuni ya simu pamoja na Airtel, Vodacom, Tigo/Zanztel.
Aidha alitumia fursa hiyo kueleza majukumu ya msingi ya Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ni kuratibu masuala ya menejimenti ya maafa nchini huku akiwaasa kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali katika mzingo wa menejimenti ya maafa ikiwemo wa kuzuia, kujiandaa, kukabili pamoja kurejesha hali pindi maafa yanatokea.
“Tumienie warsha hii kwa matokeo chanya yaliyokusudiwa kwa kuongeza ujuzi na kushirikishana uzoefu katika masuala yanayohusu fursa mbalimbali kuhusu njia sahihi za kutumia teknolojia ya simu katika mifumo na kutoa taarifa za tahadhari za awali ili kuendelea kuwa na utayari katika kukabili maafa,” alieleza Bi. Jane
Aliongezea kuwa nchi ya Tanzania imekuwa ikikumbwa na maafa ya asili na yale yasiyo ya asili ikiwemo ya mafuriko, matetemeko ya ardhi, moto, maporomoko ya tope na mawe, ukame, upepo mkali, magonjwa ya milipuko kwa binadamu na wanyama hivyo warsha hiyo ni muhimu kwa kuzingatia umuhimu wa taarifa za tahadhari za awali ili kuendelea kujiandaa kisha kukabili kwa wakati na kupunguza madhara yanayoweza kutokea wakati wa maafa hayo.
Alifafanua kuwa, taarifa za awali zinaipa jamii uelewa wa hatua za awali za kuchukua kabla ya madhara ya maafa kuwa makubwa hivyo upo umuhimu wa kuendelea kuzijengea uwezo jamii juu ya matumizi sahihi ya taarifa hizo.
Awali aliwakumbusha kuendelea kupiga namba 190 endapo kunatokea majanga, maafa au dharura ili kupata msaada zaidi kupitia Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi