December 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Elimu ya saratani yatakiwa kutolewa kwa wanawake pembezoni mwa mji

Na Mwandishi wetu, timesmajira

MTAALAMU wa Magonjwa ya Saratani kwa Wanawake na Watoto Prof. Rashmiin Aiyushman kutoka Hospitali ya Ramaiah ya nchini India,amesema katika kupambana na saratani zinazowaathiri wanawake,serikali imetakiwa kuwekeza katika miundombinu sahihi ya kuwafuata wanawake waishio pembezoni kwa kuwapatia huduma ya mkoba ya upimaji, matibabu na kinga.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati akitoa kuhusu magonjwa ya saratani zinazowaathiri wanawake yaliyoandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa),ikiwa ni muendelezo wa kusherekea siku ya Wanawake duniani katika mwezi machi,Aiyushman alisema katika kusherehekea siku ya wanawake duniani,ni muhimu kuzungumzia masuala wanayowahusu wanawake ili kuokoa watoto wanaobaki mayatima kutokana na vifo vya mapema vya wanawake vinavyosababishwa na saratani.

Amesema wasichana wadogo wanapata changamoto ya saratani hasa waliopo kwenye umri ya uzazi kati ya miaka 20 hadi 30 huku wanaume wananafasi gani ya kuangalia wakinamama katika hili kwani wanawake wanamzigo wa malezi.

Aiyushman amesema imebainika kuwa mama anapoumwa saratani huo mzigo unamuelemea mwenyewe na sio baba,hivyo elimu zaidi inatakiwa kutolewa ili kusaidia jamii katika kupambana na saratani.
“Wanawake wengi hawana elimu,hawapati huduma za vipimo na kinga dhidi ya saratani ni muhimu kwa wao kujua hali zao mapema kupitia vipimo na matibabu kwani kuna haja kuweka mifumo itakayowezesha namna ya kuwapima na kuwabaini mapema pia katika ngazi ya kijamii wapewe elimu,” amesema.

Amesema katika Bara la Asia tafiti mbalimbali zinazofanyika zinaonyesha wanawake wanaathirika zaidi na saratani ikilinganishwa na wanaume na hivyo wamewekeza zaidi kwenye tafiti ili kupata suluhisho la changamoto hiyo.

Amesema serikali zizingatie kundi la wanawake, kuwekeza elimu kwao na kupima, huduma zipewe kipaumbele na katika ngazi za maamuzi ziangalie wanawake wenye miaka 20 na 30 lakini pia lazima ionekane nafasi ya kinababa katika kuangalia wanawake wenye changamoto hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Dk Rose Reuben amesema saratani zinawapata wanawake zaidi ya wanaume na takwimu mbalimbali zinaonyesha.”Nchini India,takwimu zilionyesha saratani kuwapata wanaume zaidi, hivi karibuni baada ya kufanya utafiti wamebaini idadi ya wanawake wenye saratani inaongezeka zaidi na wametafuta taratibu mbalimbali za kuondoa hilo ombwe,”amesema na kuongeza

“Wenzetu India wanawafuata wanawake waliko pembezoni mwa mji kwa kutumia magari ambayo yanakuwa na madaktari kwa kuwafuata vituoni na hivyo kupata wanawake wenye changamoto hiyo mapema na kuwapa matibabu,”amesema.