Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Mtandao wa Polisi Wanawake wa Jeshi la Polisi (TPF-Net) Mkoa wa Mwanza umewataka
wanawake wafanyabiashara ya samaki wa soko la Kamanga jijini hapa kutosahau majukumu ya msingi ya malezi wakati wanapofanya shughuli za kuingizia kipato familia.
Mwenyekiti wa Mtandao huo mkoani Mwanza, Mrakibu wa Polisi (SP) ambaye pia ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana Virginia Sodoka,
amesema tabia za wanawake wajasiriamali kujitafutia kipato ‘fedha’ na kusahau wajibu wao katika malezi ya familia kunachangia familia kusambaratika jambo linalohatarisha usalama na kusababisha watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili.
SP.Sodoka ametoa wito huo Machi 5, 2024 wakati wanachama wa mtandao huo walipowatembelea wanawake wajasiriamali wa soko hilo kwa ajili ya kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya ‘Siku ya Wanawake Duniani’ ambayo kilele chake huadhimishwa kila mwaka Machi 8.
“Hizi pesa tunatafuta kwa shida tuwe makini, pata pesa yako badiri maisha ya familia yako ili familia ifurahie uwepo wako na utapata baraka,” amesema SP.Sodoka.
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Mwanza, Insp Faraja Mkinga amesema vitendo vya ukatili wa kijinsia vimepungua kutokana na jamii kushirikiana na Polisi kwa kutoa taarifa fiche za uhalifu.
“Endeleeni kutoa taarifa polisi za vitendo vya ukatili wa kijinsia,acheni kumaliza kesi hizo kifamilia nyumbani kwani mnawaumiza watoto wenu,”amesisitiza Insp.Mkinga.
Awali, Mkuu wa Kituo kidogo cha Polisi Mirongo jijini Mwanza, Mkaguzi
Msaidizi wa Polisi (A/Insp) Fatuma Mpinga alifafanua (bila kutaja idadi)
kwamba visa vingi vya watoto kufanyiwa ukatili ikiwemo kubakwa na kulawitiwa huchangiwa na wazazi kutotenga muda wa kuwachunguza na
kufuatilia mienendo ya watoto wao.
“Wakina mama tusiwe wasiri kwenye hili, sisi tunachangia watoto wetu kuna vitu wanafanyiwa na wakina baba hatutoi taarifa hata kama tunawapenda sana wakina baba lakini tuangalie na watoto kwani ndio taifa la kesho,”
Kwa upande wake mmoja wa wafanyabiashara wa samaki katika soko la Kamanga jijini humo, Veronica Charo amekiri kuwepo kwa wajasiriamali wanaojisahau na kutelekeza
familia jambo linalotengeneza mazingira hatarishi kwa watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili ikiwemo kubakwa na kulawitiwa.
“Tunavyoona wale watoto wa mitaani wanavyoishi tunajisikia vibaya…..,mtoto wa mwenzako ni wa kwako, unapoona amepata changamoto unaumia katika nafsi,”amesema Veronica.
Huku Lilian Charles, ameeleza kuwa baadhi ya wanawake huwatendea waume zao ukatili ikiwemo wa kuwanyima unyumba kwa
madai ya kuchoka kutokana na shughuli walizofanya siku nzima.
“Mliyosema ni kweli lakini wanaume nao wananyanyasika,muitishe kikao na wanaume nao watoe kero zao ni basi tu wao wanaishi kwa ujasiri lakini wana changamoto sana maana mwanamke anapotoka kwenye majukumu yake hataki kuguswa na mwenza,”.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi