January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwili wa aliyekuwa Ofisa Masoko Uhuru FM,waagwa

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online

MWILI wa marehemu Furaha Luhende (52),aliyekuwa Ofisa Masoko wa kituo cha redio cha Uhuru Fm, aliyefariki Februari 23,mwaka huu kwa maradhi ya moyo, umeagwa leo Februari 27,katika viwanja vya Leaders Club jijini Dar- es- Salaam na kusafirishwa kuelekea wilayani Maswa, mkoani Simiyu kwa ajili ya mazishi.

Akizungumza katika shughuli ya kuaga mwili huo Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Dar-es-Salaam, Adam Ngalawa, amesema kuwa wamepoteza mtu muhimu ambaye alikuwa mfanyakazi katika kituo hicho cha redio kinachomilikiwa na chama hicho.

“Tumepoteza mtu muhimu katika kituo na chama kwa ujumla kwa niaba ya Katibu wa CCM, Emmanuel Nchimbi na Mwenyekiti wa chama Mkoa wa Dar-es-Salaam, Abbas Mtenvu tunatoa pole zetu za dhati kwa wafiwa na hakika hatutasahau mchango wa Furaha kwetu,” amesema Ngalawa.

Kwa upande wake,Ofisa Rasilimali Watu wa kituo hicho Mkula Kitambi, ameeleza kuwa uongozi wa Uhuru Fm wanasikitika kimpoteza mfanyakazi mwenzao hivyo ofisi itahakikisha inakamilisha haraka taratibu za stahiki za marehemu na kukabidhi kwa familia.

“Kaka angu Furaha leo hii hayupo, nimebaki mwenyewe na Yesu wangu, siku moja kabla ya umauti kumkuta niliongea nae lakini alikuwa akiongea kwa shida sana, akaniambia anaumwa ,nilipomwambia niende kumuona alinizuia kuwa nisiende,kesho yake asubuhi napata taarifa ya kifo chake,”amesema Kaka wa marehemu, Derick Luhende.

Mhasibu wa ‘Club One’, Alamba Msusa, ambaye ni mmoja wa marafiki wa marehemu, amesema kwa umoja wao wana Club One wanasikitishwa na kifo hicho na kudai kuwa, siku zote ataendelea kuishi katika kumbukumbu zao.

Marehemu wakati wa uhai wake alihudumu katika kituo hicho cha redio akiwa Ofisa Masoko, hadi umauti unamkuta, ambapo kwa mujibu wa watu wake wa karibu, wanadai kuwa kwa kipindi cha hivi karibuni alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kuvimba miguu huku hali yake ikiwa imedhohofika.