Na Jackline Martin, TimesmajiraOnline, Dar
MAMLAKA ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imesema kazi kubwa iliyofanywa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia filamu yake ya Royol Tour imeongeza kasi ya watalii wanaotembelea Hifadhi ya Ngorongoro.
Hayo yamemsemwa jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Richard Kiiza, wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana wa miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt. Samia.
Amesema takwimu za NCAA zinaonesha juhudi za Rais Dkt Samia katika kufufua sekta ya utalii mara baada ya UVIKO 19 kupitia filamu ya Tanzania the Royal Tour zimechangia ongezeko kubwa la idadi ya wageni wanaotembelea Hifadhi.
Kwa mujibu wa Kiiza idadi ya watalii imefikia 752,232 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ikilinganishwa na wageni 191,614 waliotembelea Mamlaka hiyo Mwaka 2020/2021.
“Idadi ya wageni wanaotembelea Hifadhi inatarajiwa kuendelea kuongezeka zaidi na kufikia wageni 1,000,000 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 hususani, katika nusu ya kwanza ya Mwaka 2023/2024.
Hifadhi imepokea wageni 534,065 idadi hii imeongezeka kwa asilimia kumi ikilinganishwa na idadi ya wageni walitembelea hifadhi katika kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2022/2023.”Alisema,
Aidha, Kiiza amesema ongezeko la idadi ya wageni limekuwa na matokeo chanya kwenye ongezeko la mapato yatokanayo na utalii, ambapo mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka sh.bilioni 31 mwaka 2020/2021 hadi kufikia sh. bilioni 171 mwaka 2022/2023.
Aidha Kiiza alisema mapato yanategemewa kuongezeka zaidi na kufikia takribani sh. bilioni 200 kwa mwaka kwani katika kipindi cha nusu ya kwanza ya Mwaka 2023/2024 jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 123 tayari mapato yameongezeka kwa asilimia 13 ukilinganisha na mapato yaliyo kusanywa katika kipindi hicho hicho kwa mwaka 2022/23.
Pia Kiiza alisema Rais Samia alitoa pesa za Uviko 19 kiasi sh. 6,645,258,276) ambazo zilitumika kuimarisha miundo mbinu ya barabara na kununua mitambo pamoja magari makubwa ya kutengenezea barabara, kuimarisha viwanja vya ndege pamoja na miundo mbinu mingine ya utalii ili wageni waweze kufikia vivutio vya utalii kwa urahisi.
Aidha alisema Serikali imetenga kiasi cha sh. bilioni sitini na tisa kwa ajili ya kujenga tabaka gumu kipande cha barabara chenye kilomita 29.5 kutoka lango kuu la kuingilia Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro hadi Seneto nia ni kuweka tabaka gumu kipande chote cha kiliomita 83 za barabara ya kuanzia lango kuu (Lodoare gate) hadi mpaka wa Hifadhi ya Serengeti (maarufu kama golini).
Kuhusu zoezi la kuhamisha kwa hiari wananchi wanaoishi katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro, Kamishna Kiiza alisema hadi kufikia tarehe 25.02.2024 jumla ya kaya ambazo zimeshahama kwa hiari kutoka ndani ya eneo la Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ni kaya 1042 zenye watu watu 6,461 na mifugo ipatayo 29,919.
Mbali na hayo, Kiiza alisema Mamlaka Mamlaka imeweza kudhibiti matukio ya ujangili wa wanyamapori (nyamapori na vipusa) katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya eneo la hifadhi ya Ngorongoro ambapo katika kipindi husika mamlaka imeweza kudhibiti matukio ya ujangili wa tembo kutoka matukio 25 mwaka 2020/2021 hadi tukio moja mwaka 2022/2023.
“Hii imewezekana kutokana na Serikali kuiwezesha mamlaka kununua magari ya doria na vitendea kazi vingine, aidha, katika kipindi husika mamlaka kwa kushirikiana na vikosi vya kupambana na ujangili ilifanikiwa kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya dola watuhumiwa 175 wanaojihusisha na vitendo vya ujangili,” alisema Kamishna Kiiza.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa