Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Wazalishaji wadogo wa umeme ambapo amewaeleza kuwa, Serikali inawatambua na kuthamini mchango wao katika uchumi.
Hivyo wanapaswa kujiamini na kuendelea kubuni miradi mipya ya kuzalisha umeme ili nchi ipate umeme wa kutosha.
Dkt. Biteko ameyasema hayo Februari 21, 2024 wilayani Njombe mkoani Njombe, katika kikao chake na Wazalishaji Wadogo wa umeme ambacho pamoja na mambo mengine.
Wazalishaji hao walieleza changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utekelezaji wa kazi zao pamoja na njia za kuendeleza miradi hiyo.
“Nataka mtambue kuwa, Serikali haitegemei umeme kutoka vyanzo vikubwa tu kama vile Gesi au mradi wa Julius Nyerere, bali dhamira yetu ni kuendeleza vyanzo vingine ikiwemo hivi vidogo vya umeme.
“Hata kama chanzo kinazalisha kilowati moja sisi tunakithamini, hivyo mnapaswa kujiamini kwani mchango wenu ni mkubwa kwenye Sekta hii,” amesema Dkt.
Biteko
Dkt. Biteko aliwapongeza wazalishaji hao wadogo wa umeme kwa ubunifu wao ambao unasaidia katika kusambaza umeme kwenye maeneo ambayo gridi ya Taifa bado haijafika.
Pamoja na kuongeza kiwango cha umeme kwenye gridi hiyo kwani wazalishaji wengine wanaiuzia TANESCO umeme ambao unaingizwa kwenye gridi.
Aliwataka kutoogopa changamoto na kwamba Serikali itaendelea kuwaunga mkono kwa namna mbalimbali ikiwemo kuwapatia nyenzo zinazohitajika.
Ili kutatua changamoto mbalimbali zilizotajwa na wazalishaji hao wadogo wa umeme ikiwemo suala la upatikanaji wa vibali na msamaha wa kodi kwa baadhi ya vifaa vinavyotoka nje ya nchi, Dkt. Biteko ameagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuandaa andiko litakaloainisha
changamoto hizo ili ziweze kufanyiwa kazi na Serikali kwani Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka biashara ya umeme kuwa rahisi ili nchi iwe na nishati ya kutosha.
Kwa nyakati tofauti, wazalishaji hao wadogo wameishukuru Serikali kwa kuwaunga mkono kwenye kazi zao kupitia TANESCO na REA ambao wanawawezesha kwa namna mbalimbali ikiwemo ushauri wa kitaalam, fedha na vifaa ambavyo vimewawezesha kuanza kutekeleza miradi hiyo.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria kikao hicho ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, Wabunge wa Mkoa wa Njombe, Wakuu wa Wilaya na Watendaji wa Halmashauri za Mkoa huo.
More Stories
Watakiwa kupiga kura na kuondoka vituoni
Dkt.Mpango:Viongozi mtakaochaguliwa, uchaguzi wa serikali za mitaa tumieni nafasi zenu vizuri
Wananchi Nyamanoro Mashariki,Mkudi wajitokeza kupiga kura