Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
KAMATI za Siasa Kata za Buzilasoga na Mhande,wakiwemo wajumbe wa mkutano wa uchaguzi zimetakiwa kuwachangua wagombea wanaokubalika katika jamii na watakaokiwezesha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushinda uchaguzi.
Rai hiyo imetolewa na Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza,Omar Mtuwa,kwa nyakati tofauti wilayani Sengerema na Kwimba,mkoani hapa wakati akizungumza na wajumbe wa kamati hizo,kuhusu mchakato wa uchaguzi mdogo wa Udiwani ndani ya chama katika kata hizo ulioanza Februari 21,mwaka huu.
Mtuwa amewataka kujiepushe kujiingiza katika makundi yanayoweza kuigawa CCM na kuidhoofisha katika uchaguzi huo kutokana na kila mjumbe kuwa na mgombea wake badala ya mgombea ambaye hatakipa shida ya kumnadi
Amesema wajumbe wa kamati hizo za siasa pamoja na wajumbe wa mkutano wa uchaguzi wachague wagombea,wanaokubalika na wasio na makandokando katika jamii, watakaoiwezesha CCM kushinda katika uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata za Buzilasoga (Sengerema) na Mhande (Kwimba).
“Kamati ya siasa ifanye kazi yake kwa weledi kuhakikisha CCM inashinda,uchaguzi huu hautaachwa hivi hivi,taratibu zitafuatwa na ili tushinde uchaguzi huu tuepuke fitna na majungu,yawezekana viongozi wa kata mnaye mgombea wenu tofauti na anayetakiwa na wananchi mnampitisha mnayemtaka ninyi,mtakigharimu chama,ili tuwe salama tuepuke makundi yaliyopo ama tuyasambaratishe,vinginevyo mtatuletea shida,naamini hamtakuwa na matabaka,”amesema Mtuwa.
Katibu huyo wa CCM ameongeza zaidi kuwa; “Ukiwaona viongozi ndumila kuwili na wa mbea hao si wa kwetu (CCM),wanatuvuruga na kutuchonganisha katika uchaguzi,ili kazi iende salama viongozi mkubaliane lakini mkiwa na makundi mtapigwa katika uchaguzi.”
Kwa upande wake Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa, Prudence Sempa,amesema anahitajika mgombea sahihi wa kurahisisha uchaguzi na kukipatia ushindi Chama Cha Mapinduzi kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Tumekuja kuwaona ili kuwapa nguvu na tupo pamoja katika vita hii,mkifanya makosa ya kutompitisha mgombea sahihi mtazalisha makundi yatakayotusulubu katika uchaguzi wa serikali za mitaa baada ya watu kuumizana katika uchaguzi huu wa udiwani,”ameonya.
Katibu wa UVCCM mkoani Mwanza Ibrahim Kandumila amesema kazi ya jumuiya hiyo ni kuwalinda viongozi,CCM na kuhakikisha inashinda katika chaguzi mbalimbali,hivyo mgombea wao ni atakayeteuliwa kuwania kiti hicho.
Katibu wa Jumuiya ya WAZAZI,Dotto Omar amezitaka jumuiya hizo ngazi ya kata ndizo zenye jukumu hilo zisimamie uchaguzi kwa weledi.
Aidha Katibu wa UWT,Hawa Makonyola,amesema ili kurahisisha uchaguzi kamati za siasa zisipitishe wagombea kwa kufahamiana,udugu,uswahiba na makundi badala yake wamchague mtu anayekubalika na anayeuzika kwa wananchi
“Mkichagua kwa kujuana mtaufanya uchaguzi kuwa mgumu,chagueni mtu atakayekitetea Chama chetu kwa wananchi na kukipatia ushindi, watendeeni haki wana CCM wote wanaotaka kugombea lakini asiyekubalika asiteuliwe,”amesema.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika mapema Machi mwaka huu, kufuatia vifo vya waliokuwa madiwani wa kata za Buzilasoga Sengerema, David Shilinde na John Sababu wa Mhande,Kwimba ambao walifariki mwaja jana.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa