Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Urambo
WAKULIMA wa zao la tumbaku Wilayani Urambo Mkoani Tabora wamemshukuru Mkuu wa Wilaya hiyo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Elibariki Bajuta kwa kusikia kilio chao cha ukosefu wa mabani na kuwasaidia.
Akizungumza na gazeti hili kwa niaba ya wakulima wenzake, Mwenyekiti wa Chama Cha Msingi Imara-Makoye (Amcos) Ibrahimu Kagete alisema kuwa mvua kubwa zinazoendelea kunyesha wilayani humo zimesababisha mabani 217 ya kukaushia tumbaku kubomoka hivyo kuwapata hasara kubwa wakulima.
Amebainisha kuwa kubomoka kwa mabani hayo yaliyojengwa na wakulima katika kipindi hiki ambacho mavuno ya kwanza yameshaanza ni pigo kubwa kwao, kwa kuwa wangeshindwa kukausha tumbaku yao kwa wakati, hivyo kupata hasara.
‘Tunamshukuru sana Mkuu wa Wilaya kwa kuagiza kila mkulima aliyepata hasara apewe sh 200,000 kutoka kwenye AMCOS yake ili kukarabati au kujenga upya mabani yake ya kukaushia tumbaku, zoezi la uvunaji limeshaanza’, amesema.
Kagete amefafanua kuwa agizo hilo tayari limetekelezwa, AMCOS zote katika Wilaya hiyo zimewasaidia wanachama wao waliopata hasara hiyo na tayari wameanza kujenga upya mabani yao.
Aidha ameongeza kuwa wanaushirika wote wamekubaliana kuwasaidia wenzao waliopata hasara ambapo mkulima mwenye ekari nyingi zaidi atakayehitaji mabani mengi atatumia ya wenzake ili asichelewe masoko.
‘Tunaishukuru sana mama yetu, Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake wote akiwemo DC, RC, Ma DED na Wabunge kwa kujali wakulima na kuchukua hatua za haraka kuwasaidia inapotokea tatizo’, amesema
Bi.Halima Yasin mkulima, mkazi wa kata hiyo ambaye pia ni mwanachama wa Imara-Makoye Amcos ameshukuru serikali kwa kuwa karibu zaidi na wakulima na kuwaboreshea upatikanaji pembejeo kwa wakati na kwa gharama nafuu.
Amebainisha kuwa kilimo cha zao hilo kimepata mwitikio mkubwa sana kwa wakazi wa Wilaya hiyo katika kipindi hiki cha utawala wa Rais Samia kutokana na mkakati wake wa dhati wa kuinua sekta ya kilimo nchini.
Ameongeza kuwa wakulima sasa wanatembea kifua mbele kutokana na mafanikio makubwa wanayopata kupitia zao hilo na kuongeza kuwa msimu uliopita yeye binafsi alivuna zaidi ya kilo 4500 na kuuza kwa bei nzuri ya sh 6000 kwa kilo na kupata fedha nyingi.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â