January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati ya Usalama Arusha yampongeza SACP Masejo kwa kupandishwa cheo

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Kamati ya Usalama Mkoa wa Arusha imempongeza Kamanda wa Polisi Mkoani humo kwa kupandishwa Cheo hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Akitoa Pongezi hizo Mkuu wa Mkoa wa Arusha Ndugu John Mongella amebainisha kuwa kitendo cha Kamanda huyo kupandishwa cheo na Mheshimiwa Rais nikuaminiwa na kuonesha utendaji kazi mzuri ndani ya Mkoa huo ambao ni kitovu cha utalii hapa nchini .

Ameongeza kuwa Kamanda Masejo amekuwa chachu ya kuwaunganisha Askari wote kitendo kilichopelekea Mkoa huo kuwa shwari licha ya uwepo wa matukio madogo madogo ambayo yamedhibitiwa.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha ambaye amepandishwa Cheo kutoka Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) kuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Justine Masejo pamoja na kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumpandisha hicho, ameahidi kuwa ataendelea kushirikina na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili Mkoa huo uendelee kuwa shwari wakati wote.

Pia amemshukuru Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura na Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Mkoa wa Arusha kwa usimamizi wao mzuri katika utendaji wa kazi.