December 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ilala yatekeleza asilimia 95 ilani ya CCM

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Dar

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, Februari 9,2024 jijini Dar es Salaam, amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye Halmashauri Kuu ya chama hicho Wilaya hiyo.

Akiwasilisha taarifa kwa wajumbe hao, chini ya Mwenyekiti wake Said Sidde, Mpogolo amesema, hadi sasa Ilani ya CCM kwa Wilaya hiyo imetekelezwa kwa asilimia 95 kwa kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo elimu, afya,maendeleo ya jamii,biashara na uwekezaji pamoja na maliasilia na mazingira.

Amesema, miradi mingi imeshakamilika na kuanza kufanya kazi, huku akidai kuwa, nguvu kubwa imeelekezwa katika ukamilishaji wa miradi ambayo ipo katika hatua za mwisho kukamilika, akitolea mfano ukamilishaji wa kituo cha afya Kinyerezi ambacho kipo katika hatua za mwisho kukamilika.

“Ujenzi wa kituo cha afya cha Kinyerezi ambacho hivi karibuni kamati ya siasa mliweza kutembelea, kipo katika hatua za mwisho na ndani ya mwezi huu kinaenda kuanza kwani tayari tumeshapokea vifaa tiba, vitanda zaidi ya 10 vya kupumzika na 4 kwa ajili ya kina mama kujifungulia lakini pia gari ya kubebea wagonjwa”, amesema Mpogolo.

Pia, amesema upande wa elimu msingi na sekondari, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, inaendelea kuboresha miundombinu ya shule za msingi ikiwa pamoja na shule ya msingi Olympio inayojengwa kwa mtindo wa ghorofa kuongezewa madarasa mapya, huku upande wa shule za sekondari zikiwa zimekamilika ikiwemo sekondari ya Liwiti na nyingine zikiwa katika hatua za mwisho kukamilika.

Aidha Mpogolo amesema, mbali na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo, zipo athari zilizotokana na mvua zilizonyesha hivi karibuni, zilizopelekea nyumba zaidi ya 150 zilizokuwa pembezoni mwa mto Msimbazi kubomoka na vivuko ambavyo milioni 300 zimetengwa kwa ajili ya kuvirejesha vivuko hivyo.