October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi Mkuu as Bodi ya Michezo ya Bahati Nasibu( GBT), James Mbalwe akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichana)juu ya kampeni ya Mlinde Mtoto

Kampeni Kumlinda Mtoto michezo ya Bahati Nasibu yaanzishwa

Na Penina Malundo, Times Majira Online, Dar es Salaam

BODI ya michezo ya kubahatisha Tanzania (GBT) imeanzisha kampeni maalum ya miezi mitatu ambayo inalenga kuzuia ushiriki wa watoto walio chini ya miaka 18 kucheza michezo ya kubahatisha.

Kampeni hiyo iliyoanza Julai na inatarajia kumalizika Septemba mwaka huu, imeanzishwa ikiwa ni baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa watu kuwa, baadhi ya sehemu zinaendesha michezo hiyo huku watoto walio chini ya miaka 18 wakishiriki.

Mbali na kampeni hiyo pia bodi hiyo imesema, iko katika hatua za mwisho za kukamilisha mfumo ambao utasimamia mashine zote za michezo ya kubahatisha ambayo pia itaweka urahisi kuwabaini wanaoendesha shughuli hizo kinyume na sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari leo katika viwanja vya maonesho ya 44 ya biashara ya kimataifa, Mkurugenzi Mkuu wa GBT, James Mbalwe amesema, Mwaka huu watafanya utafiti ili kujua ukubwa wa tatizo hilo la mashine.

“Sasa tumeanza na kampeni ambayo itamfanya hata mtu mzima anapomuona mtoto anashiriki katika michezo hii atoe taarifa polisi au bodi ya michezo ya kubahatisha,” amesema Mbalwe.

Hata hivyo Mbalwe amesema, changamoto kubwa ipo kwa baadhi ya watu wanaoendesha biashara kinyume na utaratibu ambao huweka mashine hizo sehemu yoyote ambayo watoto pia huweza kuzitumia.

“Lakini pindi tu mfumo wetu utakapokamilika itakua ni rahisi kufuatilia mashine zote hata kama zimewekwa kwa siri zitaonekana tu,” amesema.

Katika hatua nyingine, Mbalwe amesema licha ya sekta zote kukumbwa na athari za uwepo wa virusi vya corona lakini mapato katika michezo ya kubahatisha yameanza kuongezeka kuanzia wiki ya mwisho ya mwezi Juni.

Katika wiki hiyo ya mwisho, mapato yaliyokusanywa yalifikia Sh. Bilioni nane huku akibainisha kuwa ni matumaini yake kuwa namba zitabadilika

Licha ya kuwa sekta hiyo imeanza kukua tena lakini mapato katika mwaka wa fedha 2020/2021 yatapungua kuliko matarajio yao ya awali ya kukusanya Sh. Bilioni 100.

Katika hatua nyingine ya kulinda watu wanaotembelea maonyesho ya sabasaba dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona bodi hiyo imetoa msaada wa matanki 10 na sabuni za kunawia vilivyo na thamani ya Sh. Milioni15 kwa Mamlaka ya Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TanTrade).