November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watendaji Bumbuli wakalia kuti kavu

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Lushoto

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Bumbuli wilayani Lushoto mkoani Tanga Ameir Sheiza amesema kipimo cha Ofisa Mtendaji wa Kata kuendelea kufanya kazi kwenye halmashauri hiyo ni namna atakavyoweza kukusanya ushuru na tozo kwenye kata yake.

Ameyasema hayo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani robo ya pili ya mwaka wa fedha 2023/2024 wakati wa kujadili taarifa ya kamati ya fedha,uongozi na mipango na kuongeza kuwa wanataka kuona watendaji wa kata wanakusanya mapato kulingana na shughuli za kiuchumi zinazofanyika kwenye kata zao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli Baraka Zikatimu (kushoto) akiweka saini baada ya halmashauri hiyo kuingia mkataba wa kuendesha Hoteli ya Maweni na mwekezaji Grosso Foods Co. Ltd wa Dar es Salaam

“Moja ya vipimo vya kuendelea kufanyakazi na Ofisa Mtendaji wa Kata ni kuonesha mapato ukusanyaji wa mapato ikiwemo ushuru kwenye kata yake ambaye hakusanyi mapato hayo, tutamjadili kwenye kamati ya fedha kuona anatosha kuwa na sisi au la,” amesema Sheiza.

Sheiza amesema wameweka ushindanishi wa watendaji wa kata katika ukusanyaji mapato kwenye kata zote 18 za Halmashauri ya Bumbuli nia ni kuona watendaji hao wanaongeza bidii ya ukusanyaji mapato hayo, kwani wamewapa vyombo vya usafiri ili wasikwame kwenye ukusanyaji mapato.

Akichangia kwenye taarifa ya Kamati ya Fedha, Diwani wa Kata ya Mahezangulu Rashid Sebarua, amesema gari zaidi ya 10 zinabeba miwa kwa siku kwenye kata ya hiyo lakini kwenye taarifa wameelezwa kuwa makusanyo ya miezi mitatu ni milioni 1.3, na kudai ni fedha kidogo, ukilinganisha na mapato halisi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bumbuli Ameir Sheiza (wa pili kulia) akimkabidhi kishkwambi Diwani wa Kata ya Mahezangulu Rashid Sebarua ‘Chidy’ (kushoto). Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bumbuli Hoza Mandia (wa pili kushoto), na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bumbuli Baraka Zikatimu (kulia).

Katika kikao hicho, Madiwani walipewa vishkwambi kwa ajili ya kurahisisha shughuli za halmashauri ikiwemo taarifa za vikao kwani pamoja na kwamba kutumia makaratasi ni gharama wakati mwingine wanachelewa kupata makabrasha kwa wakati.

“Tunashukuru Halmashauri ya Bumbuli kwa kutupatia vishkwambi vitatusaidia kufanya shughuli zetu kwa kisasa zaidi ikiwemo kupata taarifa mbalimbali za vikao na kwa wakati huku tukipunguza gharama ya kuchapa taarifa kwenye makaratasi,” amesema Diwani wa Dule B Ali Mkwavingwa.

Katika tukio jingine Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli imeingia mkataba wa kuendesha Hoteli ya Maweni na mwekezaji Grosso Foods Co. Ltd wa Dar es Salaam, ambapo ataendeleza na kufanya uwekezaji kwenye hoteli hiyo ambayo ni mali ya halmashauri hiyo kwa kiasi cha bilioni tatu.

Utiaji saini wa mkataba huo ulishuhdiwa na Kamati ya Fedha ya Halmashauri ya Bumbuli Februari 6,2024kwenye Ofisi ya Halmashauri iliyopo Kijiji cha Kwehangala, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Sheiza na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Baraka Zikatimu.

Wakati Sheiza na Zikatimu wakiweka saini kwa niaba ya halmashauri, Mkurugenzi Mtendaji wa Grosso Foods Co. Ltd Samira Hussein, ameweka saini kwa niaba ya kampuni hiyo ya uwekezaji.

Mara baada ya zoezi hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo akizungumza na waandishi wa habari, amesema uwekezaji wa hoteli ya Maweni iliyopo Kata ya Soni, utainufaisha halmashauri na Serikali Kuu kwa kupata kodi, ushuru na tozo, huku wananchi wakinufaika kwa kupata ajira za muda mfupi na mrefu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Grosso Foods Co. Ltd Samira Hussein akizungumza mbele ya Kamati ya Fedha ya Halmashauri ya Bumbuli kwenye hafla ya kusaini mkataba wa kuendeleza hoteli ya Maweni kati ya Halmashauri ya Bumbuli na kampuni hiyo