November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zao la Tumbaku Tabora lasomesha watoto hadi chuo kikuu

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Uyui

WAKULIMA wa tumbaku Wilayani Uyui Mkoani Tabora wameishukuru serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali, kuboresha sekta ya kilimo na kuwatafutia masoko ya kutosha hali iliyoleta neema kwa watoto wao.

Hayo yamebainishwa jana na wakulima wa zao hilo katika kata za Ibelamilundi, Isikizya na Kigwa walipokuwa wakiongea na waandishi wa habari waliowatembelea ili kujionea kasi ya Mama ilivyowanufaisha wakulima.

Lucy Kasebuye (40) mkulima mkazi wa Ibelamilundi amemshukuru Rais Samia kwa kuboresha mazingira ya upatikanaji pembejeo za kilimo kwa wakati hali iliyochochea wananchi wengi kulima zao hilo kwa kiwango kikubwa.

Amefafanua kuwa tangu ameanza kulima zao hilo miaka 7 iliyopata hakupata mafanikio makubwa sana lakini tangu Rais Samia aingie madarakani wakulima wa tumbaku wamekuwa mamilionea na wanasomesha watoto hadi vyuo vikuu.

Amesisitiza kuwa chama chao cha msingi Ibelamilundi AMCOS chenye wanachama 180 kilikuwa kimedorora kutokana na uhaba wa masoko ya kuuzia tumbaku yao lakini sasa yamekuja makampuni mengi na kuongeza ushindani wa bei nzuri.

‘Nina watoto 6, wawili wanasoma shule ya msingi, wawili sekondari na wengine wawili sasa hivi wapo Chuo Kikuu cha SAUT Mbeya, nawasomesha kupitia zao hili hili na nimejenga nyumba nzuri, tunamshukuru sana Rais Samia’, amesema.

Hussein Ramadhani (50) mkulima Mkazi wa Kijiji cha Igoko, kata ya Isikizya ameeleza kuwa awali alikuwa analima ekari 1 lakini sasa analima ekari 4 na zaidi za tumbaku, mwaka jana alivuna kilo 4500 na kupata zaidi ya sh mil 23 na msimu huu amelima ekari 5, matarajio ni kupata kilo 6000 na atauza zaidi ya sh mil 35.

‘Kwangu zao la tumbaku ni dhahabu, imenipa manufaa makubwa sana, nimejenga nyumba ya kisasa hapa hapa kijijini, nimenunua mifugo, nasomesha watoto na msimu ujao baada ya kuuza nimepanga kununua gari’, amesema.

Diwani wa Kata ya Ibelamilundi Ferdinand Magazi amemshukuru Rais Samia, Waziri wa Kilimo Hussien Bashe na Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini Almas Maige kwa kusimamia vizuri kilimo cha tumbaku, sasa limekuwa lulu.

Ameeleza kuwa wakulima wa zao hilo walikuwa wameanza kupoteza mwelekeo na wengine walishakata tamaa na kufikilia kuachana nalo lakini sasa serikali ya awamu ya 6 imeleta neema, sasa kila mwanakijiji anatamani kulima tumbaku.

Salumu Sudi (52) mkulima, mkazi wa Kijiji cha Nzigala kata ya Kigwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Msingi Kigwa Kijiji alisema kuwa wakulima wote sasa hivi wanafurahia zao hilo kutokana na masoko ya uhakika yaliyopo.

Amebainisha kuwa makampuni yote yanayonunua zao hilo yameajiri Maafisa Ugani na kuwasambaza katika Vijiji vyote ili kutoa elimu ya kilimo bora kwa wakulima, hali hii imeongeza uzalishaji wa zao hilo kila msimu na wakulima kunufaika zaidi.

Ametoa wito kwa wakulima wote kuendelea kufuata maelekezo ya wataalamu ili kuzalisha tumbaku yenye ubora unaotakiwa hivyo kujiongezea kipato zaidi na kujikwamua kiuchumi.