November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamati za ujenzi zatakiwa kujengewa uwezo kabla ya kukabidhiwa miradi

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline , Chunya

WAJUMBE wa kamati zote zinazojishghulisha na ujenzi wametakiwa kujengewa  uwezo wa kusimamia miradi mbalimbali ya ujenzi kabla ya kukabidhiwa  majukumu ya miradi ili wakikiuka utaratibu waweze kuchukuliwa hatua kwa haki na kwa mujibu wa kanuni na miongozo.

Wito huo umetolewa  leo na Mkuu wa wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji Mbaraka Alhaji Batenga  wakati alipofanya ziara ya kukagua mradi wa Zahanati ya Igundu ambao umegharimu  zaidi ya milioni hamsini (50,000,000)  ambazo zimepelekwa kujenga miundombinu mbalimbali ikiwepo tanki la maji, vinawia mikono, vyoo na kichomea taka

“Wajumbe wote wa kamati za ujenzi wajengewe uwezo wa kusimamia miradi hiyo kabla ya kukabidhiwa jukumu la kuanza kusimamia mradi husika jambo ambalo litasaidia wajumbe hao kusimamia ipasavyo mradi husika na hata kuhakikisha ukamilifu wa mradi huo” amesema Batenga

Aidha Mhe Batenga ameuagiza uongozi wa Afya kuzingatia ushauri uliotolewa na Wakala wa maji na Usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) pamoja na TANESCO ili kuhakikisha wananchi wa Igundu wanaendelee kutatua changamoto zote maana hilo ndio lengo la Serikali kusogeza miradi mbalimbali kwa wananchi wake wakiwepo wananchi wa wilaya ya Chunya

Kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya, Kaimu Mganga Mkuu Edward Tengulaga amesema  siku saba zinatosha kuhakikisha kibao kinachoonesha huduma zinazotolewa katika zahanati hiyo kinawekwa pamoja na kibao kinachoonesha uwepo wa Zahanati eneo hilo vitu ambavyo vilibainishwa kwamba ni muhimu na havikuwepo ili kuwarahishisia wananchi ambao sio wenyeji watakapohitaji huduma hiyo

Ziara ya Mkuu wa wilaya ililenga kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa katika kata ya Sangambi ambapo alitembelea pia mradi wa Maji Igundu, mradi wa ujenzi wa vyoo katika Shule ya msingi Sangambi, mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya pamoja na kukagua hali ya mazingira katika kitongoji cha Tukuyu.