Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amefungua kikao kazi cha Maofisa Utumishi wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali wanaohakiki kwa kina changamoto za walimu hususan upandishwaji wa vyeo.
Akifungua kikao hicho jana jijini Dodoma, Waziri Mchengerwa amesema katika kuhakikisha kuwa malalamiko ya Walimu yanashughulikiwa, Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais UTUMISHI iliagiza Tume ya Utumishi wa Walimu kufanya uchambuzi na kubaini walimu wote wenye changamoto katika upandaji wao wa vyeo.
“Niwapongeze Watendaji wa Tume ya Utumishi wa Walimu kwa kazi nzuri ambayo wameifanya ambapo uchambuzi umefanyika na walimu zaidi ya 136,000 wamebainishwa kuwa na changamoto,
pamoja na kazi nzuri iliyofanyika, kwa kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa malalamiko ya walimu wote yanashughulikiwa kwa ufanisi, nimeelekeza uhakiki wa kina ufanyike kwa kuhusisha taarifa za watumishi kama zilivyo kwenye Mfumo wa Taarifa za kiutumishi na Mishahara (HCMIS),” amesema
Ameagiza kushughulikia kikamilifu changamoto hizo ndani ya siku 14 na kufanya kazi hiyo kwa ufanisi wa hali ya juu ili kuhakikisha hakuna Mwalimu anayeachwa baada ya zoezi hilo kufanyika.
Wakati huohuo, Waziri Mchengerwa amewakumbusha Waajiri na Mamlaka zote zinazohudumia Walimu kusimamia vyema maslahi ya walimu ikiwa ni pamoja na kutatua kero walizo nazo.
“Naomba niweke wazi mimi sitamvumilia mtendaji yeyote ambaye hawajibiki kushughulikia kero za walimu na vilevile sitamani kusikia walimu wana malalamiko kuhusu maslahi yao ya kiutumishi,”amesema.
More Stories
Tanzania kuwa mwenyeji Mkutano wa Kimataifa matumizi bora ya Nishati
Madiwani Ilala watoa chakula kwa watoto yatima
Waziri Mkuu: Tumieni matokeo ya tafiti za kisayansi katika utekelezaji wa mipango ya kitaifa