November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madiwani Mpanda wataka matengenezo gari la taka kukamilika

Na George Mwigulu, Timesmajira Online,Mpanda
Baraza la Madiwani Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi limemtaka Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kuhakikisha matengezo ya gari la kubebea taka yanakamilika kwa haraka baada ya kuwa gereji kwa muda mrefu na kusababisha mrundikano wa taka kwenye maeneo ya kukusanyia.

Madiwani wa Manispaa hiyo hawajaridhishwa na mrudikano wa taka mitaani jambo ambalo linatishia kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ambao hivi karibuni umeripotiwa katika baadhi ya maeneo nchini.

Msitahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Haidary Sumury akifunga kikao cha uwasilishaji wa taarifa za Kata za robo ya pili ya mwaka 2023/24 kwenye Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa manispaa hiyo ameeleza kuwa wamekuwa wakipokea maelekezo kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhusu suala la taka kulimaliza kwa sababu linawachafua.

Sumury amefafanua kuwa njia ya kumaliza tatizo la takataka kuzagaa ni kuhakikisha mategenezo ya gari la kubebea taka linakamilika haraka ambapo matengezo ya gari hiyo ni pamoja na kuwekewa matairi mapya.

Jambo ambalo Msitahiki Meya huyo amebeba dhamana kwa ajili ajili ya manispaa kwenda kwa wafanyabiashara kupatiwa mataili na gari hiyo kutoka gereji.

“Tunajua magari yanapokaa gereji kwa muda mrefu likitoka tu gereji gari hilo halitakaa kwa muda mrefu barabarani kwa sababu ya changamoto zilizopo kwenye magereji kwa kuwa wako watu huko sio waadirifu kuna. uwezekano wa kubadilisha injini,”amesema.

Msitahiki Meya huyo amesikitishwa na ukodishaji wa magari kwa ajili ya kubeba taka kwa sababu gharama hizo za kukodi zingetumika kwenye matengenezo ya gari maalumu la kubeba taka liloharibika.

Vilevile amemshauri Mkurugenzi kama kuna mambo mengine ya kufanya yasimame kwa ajili ya tatizo la gari lipewe kipaumbele kwa kutengenezwa na kurudi barabarani kusaidia kwenye suala la usafi kwa sababu mazingira yaliyopo ya kupewa na viongozi maelekezo kila mahali hayapendezi.

Katika kuhakikisha tatizo hilo linakwisha baraza limetoa njia nyingine ni manispaa kutafuta kampuni ya kukopesha magari ambapo watalipa fedha kwa mkupuo mwaka ujao wa fedha kwa kuwa jambo hilo limeshaingizwa kwenye bajeti.

“Naamini tukiwasiliana na kampuni ya ukopeshaji magari tukawahakikishia kuwa tutawalipa fedha yao hata kwa awamu mbili kuanzia Agosti na Septemba inawezekana tutaingia nao mkataba na kutupa gari kwa sababu jambo hilo liko kwenye bajeti na kwa miezi hiyo tutakuwa na mapato makubwa,”amesema Sumury.

Njia nyingine baraza hilo limeshauri ni wataalamu na Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda kwenda kujifunza Halmashauri ya Wilaya ya Mlele ni mbinu gani walitumia kupata mkopo kutoka mfuko wa TAMISEMI kwa ajili ya kununulia gari.

Wande Shija,Mkazi wa Manispaa ya Mpanda Mkoa wa Katavi ameiomba serikali ya Wilaya ya Mpanda kuhakikisha suala la uzoaji taka linafanywa kwa wakati kwa sababu kuenea kwa taka ovyo kunahatarisha usalama wa afya zao.

Amesema kuwa waathirika wa taka hizo wengi wao ni watoto ambao muda mwingi wanacheza kwenye maeneo ya wazi ambako kama takataka hazitatunzwa mahali pake kuna hatari ya kuugua magonjwa ya mlipuko.