Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela hususani wa Kata ya Kirumba wametakiwa kuacha tabia ya kuzibua vyoo wakati mvua zinaponyesha ili kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.
Wito huo umetolewa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Dkt.Charles Samson wakati akitoa taarifa ya hali ya kipindupindu katika kikao cha Baraza la Madiwani cha kupokea taarifa za Kata robo ya pili mwaka 2023/24 kilichofanyika Februari Mosi,2024 wilayani Ilemela mkoani Mwanza.
Ambapo Dkt.Samson ameeleza kuwa hadi Februari Mosi,2024 Halmashauri hiyo imepata jumla ya wagonjwa 49 wa kipindupindu kati ya hao 47 wamepona na wameruhusiwa huku wawili wakiwa wapo katika kituo cha kutibu magonjwa ya mlipuko Buswelu.
“Tumepata mgonjwa wa kwanza Januari 9,2024 akitoka Kata ya Kirumba na kati ya wagonjwa hao asilimia 70 wanatokea Kata ya Kirumba sababu yote hiyo kuna shida ya wananchi kuzibua vyoo kule juu hususani mvua zinaponyesha, pia chemba za Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), zimezidiwa nyingi zinatoa vinyesi na tafasiri ya Kipindupindu ni kula kinyesi kibichi ndio maana tunahimiza kuchemsha maji kwa sababu tunaua vimelea,”ameeleza Dkt.Samson.
Ameeleza kuwa ulaji wa chakula cha moto na maji yaliochemshwa ni salama hivyo kuwataka wananchi kuendelee kuchukua tahadhari huku akitaja mitaa ilioathirika zaidi na kipindupindu ni Mlimani B,Kabuhoro, Kirumba,Kigoto,Ibanda Ziwani ,Songambele,Mihama,Laini Polisi, Kitangiri B na Jiwe Kuu.
“Madiwani tusaidie kuwaelimisha wananchi wachemshe maji na wasile vyakula vilivyo poa kwani kadri mvua zinavyozidi kunyesha kipindupindu kitaendelea kuwepo na tusipo chukua hatua za usafi kitazidi kutusumbua na kwa wagonjwa ambao wameisha toka hospitali tumewapa vidonge vya kutibu maji na kuzisafisha kaya zao kwa kutumia dawa,”ameeleza Dkt Samson.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kirumba Wessa Juma, ameeleza kuwa mfumo wa maji taka MWAUWASA wanaendelea kufanyia kazi na ukikamilika kadhia ya vinyesi barabarani haitakuwepo.
“Ni kweli wagonjwa wengi wa kipindupindu wametoka katika Kata yangu lakini serikali imeendelea kufanya jitihada za kuhakikisha wagonjwa wamepungua na kufikia mwisho,”.
Wessa ameeleza kuwa Kamati yake ya afya ya Kata na viongozi wa serikali za mitaa wanaenda mitaani kuelimisha,jamii,kuangalia vyoo na kuvikagua pia kuingia sokoni na kukemea mifumo ya kutiririsha maji machafu kwenye mitaro pamoja na kuwapiga faini watu wanaokaidi.
“Kazi kubwa tunayoifanya ni kuhakikisha kila kaya inakuwa na choo safi na salama lakini pia utiririshaji wa maji taka haukubaliki na anayefanya hivyo tunampiga faini kwa mujibu wa sheria za nchi ingawa lengo siyo faini ni kuelimisha jamii ili watu wote wafuete mfumo mzuri wa kuhakikisha maji taka yanaenda katika mfumo wake na si kila mtu kumwaga katika nyumba yake maji machafu kwa kisingizio cha kutokuwa na sinki ,kama Kata tumejipanga kudhibiti hilo na tunafanya ziara shuleni kuelimisha watoto na walimu ili kujikinga na mlipuko huo,”ameeleza Wessa.
Akifafanua kuhusu mfumo ya maji taka kuvujisha maji maeneo ya Kirumba Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) Mhandisi Robert Lupoja ameeleza kuwa mfumo wa maji taka Kirumba umekuwa na changamoto ya kurudisha maji taka kwenye makazi ya watu kutokana na mfumo huo kubeba taka ambazo siyo maji taka kwa maana ya matumizi yasiyo sahihi ya mfumo ikiwemo kwa baadhi ya kaya ambazo wamezibaini zimetega mfumo wa maji ya mvua kwenye nyumba zao na kuruhusu kuingia kwenye mfumo wa maji taka.
Vilevile kwenye mfumo huo katika maeneo ya barabara za vumbi kumekuwa na muingiliano kwa maana ya chemba za maji taka kuruhusu kupokea maji ya mvua yakiwa yamechanganyikana na udogo pamoja na mchanga hivyo kufanya kila wakati kuziba katika kipindi cha mvua kwani mifumo inakuwa imeelemewa na badala ya maji taka kusukumwa yanatoka katika nyumba za watu.
Pia ameeleza kuwa maeneo ya Kata ya Kirumba hasa katika mwambao wa mwaloni Kirumba upo chini ya levo ya ziwa kwaio mvua kidogo ikinyesha na kwa sababu mifereji ya kutoa maji ya mvua kwenye mialo kidogo imebana kutoruhusu maji mengi kuingia ziwani kunasababisha maji yanarudi barabarani na kutoa nafasi kuingia kwenye chemba za maji taka kupitia kwenye nyumba za watu na chemba.
“Kipindi hiki cha kipindupindu sisi kama mamlaka ya maji mvua inaponyesha basi tunakwenda kuzibua maji taka hatua tunayopaswa kuchukua ni kurekebisha hivyo naliomba Baraza la Madiwani,tushirikiane kuhakikisha tunafungua njia za maji hasa wakati wa mvua ili yapate muelekeo rahisi na haraka kupeleka ziwani pia tunatafuta fedha kwa ajili ya kurekebisha chemba,”.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Wakili Kiomoni Kibamba, ameeleza kuwa hali ya mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika Halmashauri hiyo imepungua tofauti na wiki mbili zilizopita kwani wamechukua hatua mbalimbali katika kukabiliana nacho ikiwemo kuimarisha usafi huku kadri mvua zinavyopungua ndivyo ugonjwa huo utaendelea kupunguza.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa