Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar
MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka watanzania kujijengea tabia ya kufanya usafi na kutunza mazingira yanayowazunguka ikiwa pamoja na kupanda miti nyumbani.
Hayo ameyasema Januari 27, mwaka huu jijini Dar es Salaam, alipokuwa mgeni rasmi wakati wa zoezi la usafi na upandaji miti lililofanyika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, lenye lengo la kuweka Jiji safi.
Mpogolo amesema, ikiwa leo ni siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, imeona ni vyema ikaadhimisha kwa pamoja siku hiyo kwa kufanya usafi katika hospitali hiyo.
Ambapo hadi sasa Serikali imeipatia hospitali hiyo kiasi cha bilioni 11 kwa ajili ya upatikanaji wa vifaa tiba huku bilioni 1 zikitolewa na Rais Dkt. Samia kwa ajili ya uboreshwaji wa huduma ya Mama na Mtoto.
“Kwa kuzingatia na kutambua umuhimu wa afya na juhudi za Rais Dkt. Samia katika sekta ya Afya…sisi kama Halmashauri ikiwa leo ni Siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Rais wetu tumeona ni vyema tukaungana nae katika kusherehekea pamoja kwa kuja kufanya usafi na kupanda miti katika hospitali hii lengo likiwa ni kuhamasisha usafi.
Hadi sasa hospitali hii imepatiwa kiasi kikubwa cha pesa kwa ajili ya uboreshaji wa huduma za afya..ambapo Bil 11 hadi sasa zimetokewa kwa ajili ya upatikanaji wa vifaa tiba na Bil 1 Rais ametoa kwa ajili ya uboreshaji wa huduma ya Mama na Mtoto.
“Kupitia hamasa hii natoa wito kwa wananchi kujijengea tabia ya kufanya usafi katika mazingira yao na kupanda miti…panda mti wa matunda au kivuli lakini mti usikosekane nyumbani kwako”, amesema Mpogolo.
Hata hivyo ameongeza kuwa siku ya leo wamepanda miti 1000 katika Kata zaidi ya nne na zoezi hilo litafanyika kwa mwezi wote huu lengo likiwa ni kupendezesha Jiji.
Aidha, ameutaka uongozi wa Hospitali hiyo kuwaondoa watu wanaolala katika eneo la geti la hospitali kwa kudai hawana makazi na wanaofanya biashara kando ya geti hilo akidai kuwa hali hiyo inashusha hadhi ya hospitali ya Taifa.
Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi, ameishukuru Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa uendeshaji wa zoezi hilo la usafi katika hospitali hiyo na kudai kuwa ni vyema wananchi wengine wakahamasika na kuwa na tabia ya kujifanyia usafi wa mwili na mazingira.
Huku akiwataka wananchi kuacha tabia ya kupendelea kula vyakula vyenye wanga na sukari kwani si salama kwa afya zao.
Pia Mkurugenzi wa Kampuni ya Usafi ya Kajenjere, Mathew Andrew, amesema” kama ilivyo shughuli zetu ni usafi hivyo hata uhamasishaji wetu ni juu ya usafi na ndiyo maana tuna mabalozi wazuri kwa ajili ya kuhamasisha masuala ya usafi…hivyo tunampongeza na kumshukuru Mkuu wetu wa Wilaya, kwa hamasa nzuri ambayo ameendelea kuifanya kwa wananchi wake juu ya masuala ya usafi na sisi tupo pamoja nae,”amesema Andrew.
More Stories
5 “best” Bitcoin Online slots games
Best Web based casinos Norway Your own #1 Norwegian Online casinos 2024
Prof. Mwakalila asisitiza uadilifu, uzalendo kwa wanafunzi wapya chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere