November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

STAMICO yatakiwa kuongeza uzalishaji wa makaa ya mawe hadi tani milioni 1

Na Moses Ng’wat, Timesmajira, Online,Ileje

WAZIRI wa Madini, Anthon Mavunde, amelitaka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuendelea kuweka mikakati madhubuti itakayowezesha kuzalishaji tani milioni moja za makaa ya mawe kwa mwaka ifikapo 2025 ili kuongeza mapato ya shirika na nchi kwa ujumla.

Mavunde ameyasema hayo, Januari 19, 2024 ikiwa ni muda mfupi mara baada ya kutembelea na kukagua mitambo ya kuchakata makaa ya mawe katika mgodi wa Kiwira-Kabulo uliopo Wilaya ya Ileje,mkoani Songwe katika ziara yake ya siku moja mgodini hapo.

“Ninawapongeza STAMICO kwa kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa makaa ya mawe ambao utapelekea kuongezeka kwa mapato ya shirika kutoka wastani wa bilioni 1 hadi bilioni 4 kwa mwezi,”amesema.

Amesema kuwa, mgodi wa Kiwira – Kabulo una hazina ya mashapo ya makaa ya mawe zaidi tani milioni 80 ambayo yakizalishwa kwa wingi ndani ya muda mfupi manufaa yake ni makubwa na kuitaka STAMICO kujipanga kuzalisha tani milioni 1 kwa mwaka ndani ya kipindi cha miaka miwili ijayo.

Ameeleza kuwa lengo la serikali ni kuona STAMICO inakuwa miongoni mwa shirika kubwa na lenye uwezo wa kushindana na mashirika mengine makubwa katika tasnia ya madini barani Afrika na duniani.

“Nataka kuliona shirika hili linakuwa kubwa zaidi kuliko hivi sasa , natamani nikiwaweka kwenye mizania na kampuni kubwa za uchimbaji madini Tanzania na Afrika na nyinyi muwe kwenye mzania huo, na jambo hili hapa STAMICO linawezekana kwani mna rasilimali na nguvu ya kutosha,” amesisitiza Mavunde.

Aidha, Waziri Mavunde amelita shirika hilo kujikita kusaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika kupitia makaa ya mawe yanayochimbwa katika Mgodi wa Kiwira – Kabulo.


“Ni dhamira ya Rais kuona nchi yetu inajitosheleza kwa nishati ya umeme, naiagiza STAMICO iende kuharakisha makubaliano mliyoingia na TANESCO na kukamilisha zile hatua muhimu za awali ili muanze mradi wa kuzalisha Megawati 200 za umeme kutoka kwenye makaa ya mawe,”.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO, Meja Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo, ameahidi kusimamia maelekezo ya Waziri Mavunde, ikiwemo ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa ya shule ya msingi Kapeta ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa urejeshaji kwa jamii.

Awali, akitoa taarifa ya mradi wa makaa ya mawe Kiwira-Kabulo, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse,ameeleza kuwa kwa sasa shirika limejipanga kutekeleza mikakati ya kulifanya liendelee kupata faida na kuendelea kuongeza mapato ya Serikali kupitia mrabaha.

Pia kupitia ada mbalimbali na gawio kwa Serikali ambapo kwa sasa wamewekeza zaidi ya bilioni 9 kwa ajili ya ununuzi wa mitambo na vifaa vya uzalishaji.

Mkuu wa Wilaya ya Ileje,Farid a Mgomi, ameipongeza serikali kwa kutoa kiasi cha bilioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 5 kutoka eneo la machimbo mpaka mgodini Kiwira.

Ambapo awali walikuwa wanazunguka kwa kutumia kilomita zaidi ya 70 kutoa makaa ya mawe kwenda kuchakatwa katika eneo la Mgodi wa Kiwira.