November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TPA yatakiwa kuhakikisha fedha zilizotolewa na serikali zinatumika ilivyokusudiwa

Raphael Okello, Timesmajira Online,Mwanza.

MKUU wa Mkoa wa Mwanza,Amos Makalla amemtaka Meneja wa Bandari Ziwa Victoria Erasto Lugenge kuhakikisha zaidi ya bilioni 18 zilizotolewa kwa ajili ya upanuzi wa bandari katika Kanda hiyo zinatumika kama malengo ya serikali yalivyokusudiwa.

Ambapo amesema upanuzi wa bandari uendane na dhamira ya ubinafsishaji wa bandari ya Dar es Salaam uliofanywa hivi karibuni.

Makalla amesema hayo Januari 19,mwaka huu kwenye ziara yake ya tatu ya kukagua miradi ya maendeleo jijini Mwanza ambapo alitaka juhudi za haraka zifanywe kukamilisha upanuzi wa ghati katika eneo la Bandari ya Mwanza Kaskazini.

Amesema kutokana na ahadi ya kukamilika kwa ujenzi wa meli ya MV Mwanza “Hapa Kazi Tu” unaotarajiwa kukamilika Mei mwaka huu inahitajika juhudi za haraka kukamilisha upanuzi wa ghati katika bandari hiyo.

Mkuu huyo wa Mkoa wa Mwanza, amempongeza Meneja huyo kwa kujitahidi kusimamia upanuzi wa bandari hizo na kwamba yeye kama mkuu wa mkoa wa Mwanza atahakikisha anasaidiana na Meneja Lugenge kutimiza adhima hiyo ya serikali katika Kanda ya Ziwa.

Hatua hiyo ya serikali kutoa fedha hizo kwa upanuzi wa bandari Kanda ya Ziwa inatokana na malengo mema ya Rais ya awamu ya sita, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha miundombinu ya usafirishaji majini.

Hata hivyo amezitaka Mamlaka za Halmashauri ya Jiji kuwatafutia sehemu za kufanyia shughuli zao wafanyabiashara hao ili wasiweze kuathiriwa na zoezi linaloendelea la upanuzi wa bandari hiyo.

Naye Meneja wa TPA Ziwa Victoria Erasto Lugenge ameahidi kufanya kazi usiku na mchana ili kuweza kukamilisha kazi kwa wakati kuendana na kasi ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayotekelezwa katika eneo hilo.