Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Wazazi wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza wametakiwa kuhakikisha watoto wao wanaripoti shule pamoja na kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili huku marufuku ikitolewa kwa watoto wenye umri wa kwenda shule kufanya kazi hususani muda wa masomo.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala wakati wa ziara yake ya kikazi yenye lengo la kukagua hali ya mahudhurio ya wanafunzi wa kidato cha kwanza na darasa la kwanza sambamba na ukaguzi wa mialo ikiwa ni pamoja na kufikisha taarifa ya ugonjwa wa kipindupindu katika Kata za Kayenze,Sangabuye na Bugogwa wilayani humo
Akikagua maendeleo ya mwenendo wa kuripoti kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza, darasa la kwanza na awali Masala amesema “Watoto ni wa kwetu sote na jukumu la kuwasomesha na kuwalinda ni letu sote kwani ni mali ya jamii,”.
Sanjari na hayo amewataka wanafunzi kuwafikishia ujumbe wanafunzi wenzao ambao wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza na hawajaripoti shule kuhakikisha wanaripoti shuleni kwani masomo yameshaanza na hakutakuwa na marudio.
“Kwa ambao hawajakamilisha mahitaji ya shule kama vile sare, madaftari wafike shule wakiwa na sare za shule za msingi hadi watakapopata lengo ni kuhakikisha wote mnasoma kwa pamoja,nasisitiza kuwa hakuna mchango wowote ambao utamuondoa mwanafunzi shuleni,”ameeleza Masala.
Pia amewahimiza wanafunzi hao kuhakikisha wanasoma na kuacha kukimbilia mambo mengine huku akiwataka kuwa mabalozi wa kusemea umuhimu wa elimu
“Wanafunzi msome, mjali sana elimu kwa sababu ndicho kimewaweka hapa elimu ni kila kitu, tumezungukwa na jamii ambayo bado inatakiwa kujua umuhimu wa elimu msikimbilie maisha kila jambo lina wakati wake,”.
Ziara hiyo ilienda sambamba na ukaguzi wa hali ya usafi wa mialo na kuongea na wavuvi na kuwafikishia taarifa ya ugonjwa wa Kipindupindu ambapo amewataka kuzingatia matumizi sahihi ya vyoo pamoja na matumizi ya maji safi na salama.
Kwa kuweka maji ya kunawa pamoja na sabuni na kuhakikisha wananchi wananawa ili kuweza kuepukana na maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu.
More Stories
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti
Ushiriki wa Rais Samia G20 wainufaisha Tanzania