November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Homera ampongeza mwekezaji kumuunga mkono Rais Samia

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

MKOA wa Mbeya umekuwa wa kwanza katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kuwa na kiwanda cha kutengeneza na kusambaza magodoro ndani na nje ya nchi.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera wakati alipoambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa kutembelea kiwanda cha magodoro cha Mbeya Foam kilichopo Iwambi jijini Mbeya.

Kwa mujibu wa Homera kiwanda hicho kimetokana na matunda ya kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

Amesema kiwanda hicho kimetoa fursa ya ajira kwa watu takribani 200, hivyo amewataka wananchi wa Mkoa wa Mbeya kumuunga mkono mwekezaji huyo, ikiwemo kununua na kutumia magodoro anayozalisha.

“Nikupongeze wewe na familia yako Kwa huu uwekezaji, umejitoa kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini, nikuhakikishie serikali ipo pamoja na wewe na itaendelea kukupa ushirikiano kadri inavyohitajika,”aamesema.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Godlisen Lyakundi amesema kiwanda hicho kimeanzishwa mwaka 2023 na magodoro yanayotengenezwa yamekidhi viwango vya kimataifa ndio maana soko lao lipo pia kwenye nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Amesema lengo la kuwekeza katika kiwanda hicho ni kuwahudumia Watanzania ili wawe na afya njema na waweze kuchapa kazi baada ya kupumzika kwenye magodoro yenye viwango.

Aidha amesema kuwa kiwanda hicho kwa kutambua umuhimu wa wazawa kimekuwa kikitoa kipaumbele cha ajira kwa vijana na watu wengine wenye rika tofauti.