November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Taasisi kufanya uchechemuzi haki za upatikanaji umiliki ardhi

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Taasisi ya MyLEGACY imejipanga kufanya uchechemuzi wa kubadili fikra na mitizamo lakini pia kuwajengea uwezo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili waweze kuwa na uelewa na taarifa sahihi za umiliki ardhi.

Pia imejipanga kutoa ushawishi kwa makundi hayo matatu kushirikishwa katika utoaji maamuzi kwenye ngazi zote za familia, mabaraza ya ardhi n.k

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya MyLEGACY Fortunata Temu wakati akizungumza katika mkutano wa wadau,  uliokuwa na adhma ya kujadili namna ya kufanya uchechemuzi wa haki za wanawake, vijana na watu wenye ulemavu za kujipatia makazi bora lakini pia ardhi na Haki za umiliki wa mali 

“Sisi kama MyLEGACY tunatekeleza mradi ambao unalenga katika kuboresha mazingira ya kujifunzia pamoja na mazingira ya kuishi na katika kufanya hilo tumeona ni lazima tuelewe Hali halisi ya makundi haya ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu”

“Bado uhitaji wa Elimu upo kwenye jamii hivyo wadau waendelee kuhakikisha wanafanya uchechemuzi na kushirikisha jamii kuhusu haki ya umiliki wa ardhi na kujua wapi wanaweza kwenda kudai haki zao”

Amesema katika tafiti walizozifanya changamoto kubwa walizozibaini na wamepanga kuzifanyia kazi ni suala la fikra na Imani ambazo watu wanazo katika makundi hayo matatu.

“Kuna watu Wana mitazamo ya kwamba, mwanamke hawezi kumiliki mali ikiwa ni pamoja na ardhi, kijana nae anategemewa kufanya kazi kwenye ardhi ya wazazi na fikra ni kwamba atakuja kurithi na watu wenye ulemavu fikra za watu ni kwamba mtu mwenye Ulemavu ni wa kusaidiwa tu”

Temu amesema hadi sasa, bado kuna uelewa mdogo wa haki za kisheria katika makundi hayo.

“Pamoja na kwamba sheria zipo nzuri zinazoweza kuwafanya , wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wakapata ardhi lakini kama wewe mwenyewe haujui haki zako na sheria zinasema nini itakua ni ngumu kupaza sauti na kudai haki zako”

Kuhusu suala la kiuchumi, Temu  amesema ili uweze kurasimisha ardhi na uweze kupata hati miliki, zinahitaji gharama,  ambapo makundi hayo matatu kwa asilimia kubwa hayawezi kumudu gharama kwasababu uchumi ni mdogo.

Naye Mtaalamu wa masuala ya ardhi kutoka shirika la LANDESA, Khadija Mrisho, amesema wanawake wanakutana na changamoto nyingi kwenye masuala ya umiliki na kupata ardhi ikiwemo changamoto za mifumo lakini pia Mila na desturi ambazo nyingi ni kandamizi hivyo aliwataka wadau kuendelea kuwa pamoja kuhakikisha kwamba wanafanya kazi kuondoa changamoto ambazo zinamnyima mwanamke haki yake ya kumiliki ardhi.

Akiwasilisha taarifa ya utafiti alioufanya kwaajili ya shirika la MyLEGACY, Wakili Mtafiti wa wakili wa kujitegemea, Clarence kipogota amesema utafiti huo ulihusiana na Hali ya umiliki Mali hususani ardhi na nyumba kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu Tanzania ambapo waligusia kwenye mikoa ya Dar es Salaam,  Kilimanjaro na Mwanza kwa kutazama namna gani mifumo ya kisheria, kisera na utendaji wake unawezesha au unakwaza makundi hayo kuweza kumiliki Mali hizo.

“Katika utafiti wetu tulibaini kwamba nchi inasheria na sera nyingi za kuratibu masuala ya ardhi kiujumla ikiwa ni pamoja na kutoa ulinzi katika masuala ya ardhi, katika upande wa ardhi kuna sheria za mwaka 1999 zinazobainisha bayana kwamba mwanamke na mwanaume wanahaki sawa ya kumiliki Ardhi”

“Kwa upande wa nyumba tumeona kuna mapungufu, hatuna sheria maalumu inayosimamia masuala ya nyumba mbali na Ile inayoanzisha na kuratibu shughuli za shirika la nyumba la Taifa ambalo Lina sheria yake mahususi ya mwaka 2022 ambapo mbali na hiyo hakuna sheria nyingine tofauti na zilivyo nchi nyingine”

Pia amesema suala la ulinzi wa Mali hizo walibaini kwamba watu wengi hawana hati miliki za ardhi na nyumba ambapo asilimia 60 ya watanzania waliowafanyia mahojiano hawana hati miliki za ardhi hivyo hawawezi kupata fursa za kiuchumi ambazo wangeweza kuzitumia katika kumiliki ardhi kama kupata mikopo katika Taasisi za kifedha n.k

Amesema suala la ushiriki wa wanawake na vijana na watu wenye ulemavu katika vyombo vya maamuzi yanayohusiana na umiliki na usimamizi wa masuala ya ardhi ambapo asilimia 10 ya wanawake ndiyo walisema wataongeza wanashirikishwa sana katika maamuzi yanayohusiana na ardhi na nyumba katika ngazi za familia .

“Sheria zitekelezwe jinsi zinavyotamka na Tanzania tuwe na sheria maalumu inayoratibu nyumba za stahad distance houses lakini pia upatikanaji mikopo , kwani asilimia 39 ndiyo wanaotafuta mikopo katika Taasisi za kifedha maeneo ya mjini “