Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Takribani watu 80 wameripotiwa kuumwa ugonjwa wa kipindupindu tangu Mkoa wa Mwanza ulivyoripotiwa kuwa na mlipuko wa ugonjwa huo Januari 4,2024 huku wito ukitolewa kwa jamii kuwa na vyoo na kuzingatia matumizi yake kwa usahihi.
Akizungumza wakati akifunga semina ya siku moja juu ya mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kwa waandishi wa habari jijini Mwanza iliofanyika Januari 16,2024, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Thomas Rutachunzibwa amewataka waandishi wa habari kuendelea kushirikiana na ofisi yake kwa kuelimisha jamii ili kujikinga na ugonjwa huo.
Kwa kila kaya kuwa na choo na kukitumia kwa usahihi,kunawa mikono kwa maji safi na salama yanayotiririka kabla na baada ya kula au kutoka chooni na kuhakikisha anakula chakula cha moto.
“Tuhakikishe kila kaya inatumia maji ambayo yapo katika chombo safi na salama,yachemshwe na kuchujwa na kitambaa safi na yawekwe kwenye ndio ambayo ina koki hatushauri sana kikombe cha kuchotea kinaweza kuleta madhara kwani maji yanaweza kuchafuka tena,”ameeleza Dkt Rutachunzibwa.
Pia ameeleza kuwa mkakati mwingine katika kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo ni kuhamasisha jamii kunywa maji yaliotibiwa kwa kutimia kidonge kinachosambazwa kwa sasa kinachojulikana kwa jina la Aqua tabs.
“Kidonge hiki kinatumika kutibu maji ya ndoo ya lita 10 kidonge kimoja na kwa ndoo ya lita 20 vidonge viwili kisha unatikisa ili kuchanganya maji vizuri kidonge hichi kinatakiwa kuhifadhiwa sehemu isiyokuwa na mwanga mkali kwakuwa kikiachwa hapo kinaweza kusababisha madhara mengine ya kiafya,” amesema Dk Ruchunzibwa.
Aidha wanasisitiza ulaji wa chakula cha moto na wanaopenda kula mahindi ya kuchoma barabarani ni vyema yakawa ya moto na si ya baridi kuchukua hatua kama zile zilizofanyika kipindi cha UVIKO-19.
Sanjari na hayo wanashauri kwenye jamii unapotokea msiba ni vyema kuita wataalamu wa afya ili kujiridhisha kifo kimetokana na nini,ili ikithibitika ni kipindupindu maziko yatafanyika chini ya usimamizi wa wataalamu ili kuepusha jamii kusafisha na kugusa mwili ambayo inaweza kuwa hatari kupata maambukizi.
“Kukitokea msiba ambao sababu zake zina mashaka waite wataalamu waweze kufanya tathimini hicho kifo kimetokana na nini kipindupindu au la,lakini misiba yote ndani ya Mkoa wa Mwanza,tukimaliza kuzika watu watawanyike kwani hali yamikusanyiko kwenye misiba ni moja ya kichocheo cha maambukizi kusambaa, kwenye mikusanyiko mingine kama nyumba za ibada kuwe na maji safi yanayotiririka na sabuni kuwe na vyoo safi wakati wote na watu wanatumia vyoo hivyo wavitumie vizuri katika hali ya usafi,”ameeleza Dkt.Rutachunzibwa.
Kwa upande wake Ofisa kutoka Wizara ya Afya Emmanuel Mnkeni ameitaka jamii kuzingatia usafi wakati wa maandalizi ya kupika chakula,kuosha matunda na mbogambiga kwa maji moto.
“Ili kudhibiti mlipuko wa kipindupindu Usafi wa mazingira unapaswa kuzingatia na kuwa sahihi huku waandishi wa habari mkielimisha jamii juu ya kutumia vyoo kwa usahihi na usafi pia,”ameeleza.
Naye Yusuph Yusuph kutoka Wizara ya Afya akijibu maswali yalioulizwa na waandishi wa habari ameeleza kuwa jamii inapaswa kuondoa dhana potofu kuwa kuweka maji kwenye friji au kuyaacha kwenye ndoo kwa muda mrefu yanasababisha wadudu kuganda na kufa kuwa sio kweli badala yake wanasinyaa na iwapo mtu atatumia maji yenye vimelea hivyo atakuwa hatarini kupata dalili za kipundupindu.
“Kwahiyo tusidanganyike kuwa kuweka maji kwenye friji kunaua wadudu hao hapana, tunachoshauri ni mtu kuchemsha maji na kuyahifadhi vziuri kabla ya kuyatumia,” amesema.
Akitoa elimu kwa waandishi wa habari, Mratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma Mkoa wa Mwanza, Renard Mlyakado, ameeleza kuwa ugonjwa wa kipindupindu una ambukizwa kwa kunywa maji au kula chakula kilichochafuliwa na kinyesi chenye bakteria wa maambukizi ya ugonjwa huo.
Mlyakado ameeleza kuwa dalili za ugonjwa huo huanza kuonekana ndani ya masaa 24 hadi siku tano baada ya kuambukizwa, dalili hizo ni Kuharisha maji maji yanayofanana na maji ya mchele, Kutapika, Kujisikia mlegevu na kukosa nguvu, kusikia maumivu ya misuli,upungufu wa maji mwilini pia ngozi kusinyaa, midomo kukauka, macho kudumbukia ndani.
More Stories
Watakiwa kushirikiana kutikomeza matatizo ya lishe
CCBRT yazidi kuunga mkono juhudi za Rais Samia
Madaktari bingwa wa Samia watua Rukwa