Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Songwe
MFANYABIASHARA maarufu wa pembejeo za kilimo mkoani wa Songwe, William Lema na wenzake watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Songwe wakikabiliwa na mashitaka 10, yakiwemo ya kuhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo namba 1211 ya mwaka 2024 ni Omary Hashimu, ambaye alikuwa muajiriwa wa muda wa kampuni ya mawasiliano ya simu za mkononi Vodacom, Camilius Honde mshitakiwa namba tatu ambaye ni wakala wa kampuni ya mawasiliano ya Tigo pamoja na Robert Mrema ambaye ni mshtakiwa namba nne.
Hata hivyo, mshitakiwa namba moja Lema hakuweza kuhudhuria mahakamani hapo baada ya Wakili wake Isaya Mwanri kutoa udhuru mahakamani hapo kuwa mteja wake asingeweza kufika baada ya kuugua na amaelazwa hospitalini akiwa mahututi.
Akisoma hati ya mashitaka mahakamani hapo Januari 16,2024, Wakili wa Serikali Mkoa wa Songwe, Joseph Mwakasege mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube, amedai kuwa katika eneo la Mlowo, wilayani Mbozi katika msimu wa kilimo wa 2022/23 na 2023/24 washitakiwa waliongoza genge la uhalifu na kujinufaisha.
Katika shitaka la pili linalowakabili mshitakiwa namba moja na namba mbili (Lema na Hashimu) washitakiwa wanadaiwa kuingilia mfumo wa mbolea ya ruzuku na kuingizia serikali hasara ya bilioni 1.86.
Wakili wa Serikali Mwakasege ameeleza mahakamani hapo kuwa, vitendo wa washitakiwa hao kuingilia mfumo wa serikali wa ruzuku ya mbolea walifanikiwa kujinufaisha na kujipatia mifuko ya mbolea ya ruzuku 1793 iliyokutwa kwenye hifadhi (ghala) la mshitakiwa namba moja Lema.
Aidha, washitakiwa hao wanadaiwa kukwepa kodi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ikiambatana na shitaka lingine la kushindwa kutoa risti (stakabadhi) za kielektroniki ili kuhalalisha biashara yao.
Katika shitaka la sita, lililowahusisha washitakiwa namba mbili na tatu (Hashimu na Honde) linahusu kuingilia mfumo wa mawasiliano ambapo ni kinyume na makosa ya kimtandao namba 14 ya mwaka 2015, huku shitaka la saba ni kuingilia mawasiliano ya simu ya mtu mwingine kwa lengo la kurahisisha kutenda uovu wao.
Wakili Mwakasege alieleza mahakamani hapo kuwa, shitaka la nane lilimhusu mshitakiwa namba tatu ambaye ni Honde ambaye akiwa kama wakala wa kusajili laini za simu katika kampuni ya simu ya Tigo, licha ya kampuni hiyo kufunga mfumo wa kusajili wakulima yeye aliendelea kubaki kwenye mfumo na kuendelea kuingiza wakulima katika mfumo huo kinyume cha sheria.
Pia mshitakiwa huyo anadaiwa kutoa taarifa za uongo kwenye mfumo wa ruzuku ya mbolea, akidanganya kuwa ana mashamba na kunufaika kwa kujipatia mifuko 5,000 mbolea ya ruzuku.
Shitaka la 10 liliwahusisha washitakiwa wote wanne ambapo wanadaiwa kutakatisha kiasi cha milioni 373 baada ya kufanya miamala ya milioni 455 na kulipa kodi TRA kiasi cha milioni 81 tu.
Hata hivyo, washitakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 30, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa tena na washitakiwa wote watatu waliokuwepo mahakamani hapo walirejeshwa mahabusu.
Kabla ya Hakimu Makube kuahirisha kesi hiyo, Wakili wa washitakiwa namba moja na nne (Lema na Mrema) Mwanri alitoa hoja mahakamani hapo kwa kueleza kuwa washitakiwa wameshitakiwa kwa makosa yasiyo dhaminika hasa ya utakatishaji fedha, aliisihi Jamhuri kuharakisha upelelezi ili kesi hiyo iendelee kusikilizwa kwa utaratibu unaotakiwa na Mahakama.
More Stories
5 “best” Bitcoin Online slots games
Best Web based casinos Norway Your own #1 Norwegian Online casinos 2024
Prof. Mwakalila asisitiza uadilifu, uzalendo kwa wanafunzi wapya chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere