Na Agnes Alcardo, Timesmajira. Online. Dar
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Januari 10, 2024 amefanya ziara makao makuu ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) jijini Dar es Salaam.
Lengo ya ziara hiyo ni kuipongeza Mamlaka hiyo kufuatia ukamataji wa dawa za kulevya zaidi ya Tani 3, zilizokamatwa Disemba, 2023.
Akizungumza na Maafisa wa DCEA, Waziri Majaliwa, amesema Serikali inathamini kazi kubwa inayofanywa na mamlaka hiyo katika kupambana na dawa za kulevya, huku akidai kukamatwa kwa dawa hizo ni ushindi mkubwa katika vita ya kupambana nazo.
“Nimekuja kuona mwenyewe zile dawa mlizokamata. Lakini pia kuwapongeza kwa kazi nzuri mliyoifanya, mafanikio haya yanaanza kuleta sura ya kwamba Tanzania si mahali sahihi kwa kuzalisha, kusafirisha, kuuza na sio mahali pazuri kwa Matumizi ya Dawa za kulevya,” amesema Majaliwa.
Ameitaka Mamlaka hiyo kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kuhakikisha dawa za kulevya zinatokomezwa nchini, huku akiahidi kuwa, Serikali itaendelea kuiwezesha mamlaka hiyo, iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
“Nawaomba Mamlaka muendelee kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha kuwa dawa za kulevya zinatokomezwa nchini na sisi kama Serikali tutaendelea kuiwezesha mamlaka hii ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi,” ameongeza Majaliwa.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo amemshukuru Waziri Majaliwa na serikali kwa ujumla, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha Mamlaka kufanikisha kazi zake.
“Naomba kukushuru wewe Waziri Mkuu kwa kuendelea kuisimamia mamlaka katika kutekeleza kazi zake vizuri chini ya maelekezo na maagizo yako ambayo unayatoa mara kwa mara kupitia kwa wasaidizi wako.
“Sisi kama watumishi tunahakikisha tunatekeleza maagizo yako kwa weledi na ufanisi mkubwa ili kuhakikisha malengo ya Tanzania bila dawa za kulevya inawezekana na kuwa salama,” amesema Lyimo.
Disemba mwaka jana, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilikamata dawa za kulevya zaidi ya tani 3 katika eneo la Kibada, Dar es Salaam, dawa hizo ni aina ya Heroin na Methamphetamine, ambapo kiwango cha dawa hizo za kulevya ni kikubwa ambacho hakijawahi kukamatwa nchini, tangu shughuli za udhibiti zianze kufanyika.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi