November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mahundi; wanasiasa wasipotoshe wananchi, huduma ya maji inalipiwa

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Lushoto

NAIBU Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi amewataka wanasiasa wasije kuwaposha wananchi juu ya huduma ya maji,badala yake wawaeleze ukweli kuwa huduma hiyo inalipiwa ili miundombinu ya maji iweze kuwa endelevu.

Amesema ni kweli maji ni ya Mungu lakini yakichakatwa ili kuwafikia wananchi kuna gharama ambazo tayari zimebebwa na Serikali kwa kupeleka miradi ya maji kwa wananchi ili iwe endelevu wananchi lazima walipie.

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi akitoa maagizo alipofika kwenye Mradi wa Maji Funta uliopo Halmashauri ya Bumbuli.

Mhandisi Mahundi amesema hayo Januari 8, 2024 alipofanya ziara ya kukagua miradi ikiwemo mradi wa maji Funta na Wanga iliyopo Halmashauri ya Bumbuli mkoani Tanga, baada ya kuelezwa na viongozi wa Bodi za Maji kuwa wananchi wanataka kunywa maji bure, kwani hata sh. 1,000 kwa kaya kulipia kwa mwezi wanaona ugumu.

“Serikali imedhamiria kupeleka maji kwa kila kijiji na kitongoji na ifikapo mwaka 2025, maji hayo yapatikane kwa asilimia zaidi ya 85,tukiweka maji hayo John atafungua koki hiyo, Hassan atafungua koki hiyo, Halima atafungua koki hiyo, mara ng’ombe amepita, amepiga pembe koki hiyo, hivyo itavunjika,”amesema Mhandisi Mahundi.

Ambapo ameeleza kuwa ili kuweza kununua koki nyingine na mabomba yaliyoharibika au kuwa chakavu, itabidi wachangie.

“Kila familia ikichangia sh. 5,000 (Mwangozo wa Wizara maji ya mtiririko), mradi utakaa hadi miaka 50 au 100,hivyo, viongozi wa kisiasa waseme ukweli kwa wananchi kuwa maji yanalipiwa, wasitake kujitengenezea mazingira ya kuchaguliwa kwa kupotosha wananchi kuwa wasilipe… usiseme sh. 1,000 sitoi, mradi utakufa,”amesema Mhandisi Mahundi.

Pia amesema wanataka wananchi wachangie huduma ya maji kutokana na makubaliano kwenye vikao vyao vya vijiji vilivyoamua ama kupanga vikishirikiana na Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO’s).

Wananchi wa Kijiji cha Wanga, Kata ya Mgwashi, Halmashauri ya Bumbuli wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi.

Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga, amesema mradi wa maji Funta ulianza rasmi Agosti 18, 2022 ulipaswa kukamilika ndani ya siku 270, unatarajiwa kuhudumia wananchi 4,782 kwenye vijiji vya Funta na Manga na sasa upo asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika Aprili 30, mwaka huu.

Mhandisi Sizinga amesema utekelezaji wa mradi wa maji Wanga ulianza Agosti 18, 2022, na ulipaswa kukamilika ndani ya siku 270,unatarajiwa kuhudumia wananchi 2,339 wa vijiji vya Wanga na Kwemkole, na unatarajiwa kukamilika Aprili 30, mwaka huu.