November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waamuzi Elly Sasii, Sudi Lila na Mbaraka Haule wanafungiwa miezi mitatu kwa kosa la kutokuumudu mchezo uliochezwa Juni 21, 2020 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Adhabu hii imetolewa kwa uzingativu wa kanuni ya 39(1) kuhusu udhibiti wa waamuzi.

Mechi ya Yanga, Azam yamponza Sasii, wenzake

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

MWAMUZI wa kimataifa mwenye beji ya FIFA, Elly Sasii na wasaidizi wake, Soud Lila na Mbaraka Haule wamefungiwa kutochezesha kwa muda wa miezi mitatu kwa kosa la kutokuumudu mchezo namba 300 wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara (VPL) uliochezwa Juni 21 kati ya Yanga na Azam FC.

Mara baada ya mchezo huo kumalizika zilisikika kelele nyingi kutoka kwa baadhi ya mashabiki waliokuwepo uwanjani hapo pamoja na wadau mbalimbali wa soka ikiwemo wachambuzi wakikosa maamuzi hayo wakidai Azam walinyimwa magoli mawili na penalti moja huku Yanga nao wakinyimwa penalti moja.

Kufuatia kitendo hicho, uongozi wa klabu ya Azam kupitia kwa Mtendaji Mkuu wa wake Abdulkarim Amin ‘Popat’ waliandika barua kwenda kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi la Ligi Tanzania Bara (TPLB), ikieleza kutoridhishwa na maamuzi yaliyotpolewa katika mchezo huo.

“Malalamiko haya yanatokana na nafasi tulizotengeneza kukataliwa kipindi cha kwanza dakika ya kwanza baada ya mpira wa krosi y Idd Suleiman ‘Nado’ na goli kufungwa na Abdallah Kheri kukataliwa, nafasi ingine ilikuwa dakika ya 47 ya Idd Suleiman aliyetoa pasi kwa Never Tigere na goli kupatikana, lakini nafasi hizi mbili waamuzi walitafsiri ya kuwa wachezaji wetu walikuwa katika nafasi ya kuotea,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa, si hivyo tu kwani hata dakika ya 75 beki wao Mganda, Nico Wadada aliangushwa ndani ya eneo la penalti lakini cha kushangaza mwamuzi hakutoa penalti.

“Haya matukio yamekuwa yakijirudia, tunaomba uchunguzi ufanyike na haki itendeke kwa mujibu wa sheria, tunajua makosa mengine yanakuwa ni ya kibinadamu, ila tunaomba haki itendeke. Kuna vipande vya video vya mchezo huo kwa kujiridhisha tunavituma ili Kamati yako husika ivipitie na kutoa maamuzi,” ilimalizia taarifa hiyo.

Lakini baada ya kupokea malalamiko hayo, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi katika kikao chake cha Julai 2, iliamua kutoa adhabu hiyo kwa kuzingatia kanuni ya 39(1) kuhusu udhibiti wa waamuzi.

Mbali ya waamuzi hao kufungiwa, lakini pia klabu Yanga imepigwa faini ya Sh. 500,000 kwa kosa la mashabiki wake kuwarushia chupa za maji wachezaji wa Namungo walipokuwa wanashangilia baada ya kufunga goli la pili Juni 23 Uwanja wa Taifa katika mchezo huo uliomalizka kwa timu hizo kutoka sare ya 2-2.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya TPLB, tukio hilo lilitokea baada ya wachezaji wa Namungo kushangilia na kupita karibu na walipokaa washabiki wa Yanga na adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 43(1) ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti wa Klabu

Pia Azam FC imepigwa faini ya Sh. 500,000 kwa kosa la wachezaji na maofisa wa timu hiyo kuingia uwanjani kwa kupitia mlango tofauti na ulioandaliwa katika mechi ya Ligi Kuu namba 315 dhidi ya Biashara United FC iliyochezwa Juni 23.

Taarifa hiyo imedai kwamba Azam FC walitoa kisingizio kwamba walizuiwa kuingia kupitia mlango ulioelekezwa ingawa hakuwasaidia kuepuka adhabu iliyotolewa kwa mujibu ya kanuni ya 14(49) kuhusu taratibu za mchezo.