November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waganga wa kienyeji watakiwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kuzuia mauaji

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Waganga wa tiba asili(kienyeji) wametakiwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kuzuia matukio ya mauaji yanayotokana na imani za kushirikiana na ya kujichukulia sheria mkononi, migogoro ya ardhi,wizi pamoja na unyang’anyi wa kutumia silaha.

Rai hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Wilbrod Mutafungwa wakati
akizungumza Desemba 21, 2023 kwenye mkutano wake na Waganga wa Tiba asilia zaidi ya 500 uliofanyika mkoani humo.

Ambapo SACP Mutafungwa amewataka wataalamu hao kwenda kutoa elimu kwa jamii inayowazunguka ili kuhakikisha wanapunguza matukio ya mauaji na uhalifu.

“Tufike hatua matukio ambayo yanakuwa yakileta hofu katika jamii yetu yanaisha mfano mauaji yanayotokana na imani potofu za kishirikina, migogoro ya ardhi, matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watoto, kuwania mali, unyang’anyi, wizi, pamoja na utapeli na ndio maana tumewaita leo ili kuzungumza na kuona namna gani mnaweza kusaidia katika kupunguza vitendo hivyo kwa sababu nyie ni kundi muhimu,” amesema Mutafungwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Upelele wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mwanza, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Yesaya Sudi amewaasa waganga wa tiba asilia kuwafichua waganga bandia wa tiba hiyo na wapiga ramli chonganishi katika jamii kwani ndio chanzo cha kuchafua sifa ya taaluma hiyo.

“Ukibaini mtu ambaye anapiga ramli chonganishi usimuache salama kwa sababu atakuwa anachafua kundi lenu pia mkiona mtu hana cheti wala taaluma ya tiba hiyo toa taarifa mapema ili asije kuwachafulia kundi lenu,” amesisitiza SSP. Sudi

Naye Mwenyekiti wa Waganga wa tiba asilia Mkoa wa Mwanza, Shabani Ramadhani akizungumza kwa niaba ya kundi hilo ametoa wito kwa waganga wenzake kutoa taarifa ya waganga wl wasiofuata sheria huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu Hospitali za Rufaa kuwa na kitengo cha tiba asilia.

“Niwaombe waganga wenzangu wa tiba asilia tusivunje sheria za nchi, tujiendeleze kielimu katika vyuo vya waganga wa tiba asilia,serikali na Jeshi la Polisi mzidi kutoa elimu hii msiishie mjini tu bali ifike hadi vijijini kwa sababu huko wengi wao hawajawai kufikiwa na elimu kama hii tunayopatiwa,” amesema Ramadhani.

Kuhusu hali ya ulinzi na usalama mkoani Mwanza, Kamanda Mutafungwa amesema Jeshi la Polisi lipo imara na limejipanga vizuri kuhakikisha linawasimamia na kuwaelekeza wananchi na ikiwezekana kuchukua hatua za kisheria kwa watakao fanya uhalifu kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka 2023.