November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bilioni 23 za TACTIC kujenga soko na stendi ya kisasa Bukoba

Ashura Jumapili, Timesmajira Online,Bukoba.

Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba imepewa kiasi cha bilioni 23 kati ya tilioni moja za mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Miji Tanzania ( TACTIC )kwa miradi ya soko, stendi kuu,barabara za mitaa kilomita 7 na ujenzi wa kingo za mto Kanoni.

Huku Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Serikali za Mitaa (TAMISEMI )Mohamed Mchengerwa amewaonya viongozi wa kisiasa na serikali watakaofanya hujuma na ubadilifu katika mradi wa ujenzi wa stendi kuu ya mabasi Bukoba na kusisitiza kuwa hatawaonea aibu atawachukulia hatua kali za kisheria.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Serikali za Mitaa TAMISEMI , Mohamed Mchengerwa akizungumza na wananchi na viongozi alipotembelea Soko Kuu na Stendi Kuu ya mabasi Bukoba

Mchengerwa,ameyasema hayo wakati akikagua eneo la mradi wa stendi ya kuu ya kisasa ya mabasi yenye ukubwa wa hekari 14 Mjini Bukoba mkoani Kagera.

Amesema Msimamizi Mkuu wa mradi huo ni Wakala wa Barabara Mijini na Vijini ( TARURA ) kwa sababu wanataka kubadilisha Mkoa wa Kagera kuwa wakuvutia.

“Yeyote atakaeingiza mkono kwenye mradi huu wa ujenzi wa stendi nitashughulika naye bila kujali nafasi yake iwe ya kisiasa au mtumishi wa serikali nitamuondoa akiwa juu yangu nitamuomba Rais amuondoe ili asiendelee kukwamisha shughuli za maendeleo katika Mji wa Bukoba,”amesema waziri Mchengerwa.

Hivyo amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba Hamid Njovu kuongeza vyanzo vya mapato kwa sababu vilivyopo sasa ni vya zamani na ukusanyaji wa mapato uko chini ili Bukoba iwe ya mfano katika maendeleo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba Hamid Njovu wa kwanza kushoto

Aidha,alipotembea Soko Kuu la Bukoba linalotarajiwa kujengwa upya na kuwa la kisasa alimtaka Mkurugenzi wa Manispaa hiyo katika mpangilio wa ujenzi kuwafikiria kwanza wafanyabiashara waliokuwepo na kuondolewa kinyume na taratibu,waliopo sasa pia kuhakikisha wafanyabiashara wote waliopo nje ya soko wanaingia ndani.

Pamoja kuhakikisha anawatafutia wafanyabiashara hao eneo zuri la kufanyia biashara wakati wakipisha ujenzi wa soko la kisasa na vibanda vijengwe kulingana na mahitaji ya wafanyabiashara wote katika soko hilo.

“Msiwafukuze wafanyabiashara sokoni watafutieni eneo mbadala la biashara wakati wanapisha ujenzi wa soko la kisasa na taratibu zote zikikamilika za michoro na mkandarasi akipatikana ujenzi uanze mara moja,”amesema Mchengerwa.

Sanjari na hayo amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali katika miradi mikubwa inayotekelezwa katika maeneo yao.

Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba Hamid Njovu,amesema soko hilo linahudumia wanunuzi elfu 10,000 kwa siku na lina wafanyabiashara 1,400 ambalo lina ukubwa wa eneo la mita za mraba 11,403.

Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Kagera

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Hajath Fatma Mwassa,amesema wananchi wa Bukoba wataondokana na adha ya stendi yenye tope ambayo imekuwa kero kwa zaidi ya miaka 40.

Hivyo kupitia TACTIC wananchi wanashukuru kwa miradi mikubwa inayotekelezwa Bukoba ambayo haijswahi kutokea tangu Uhuru.

Wananchi
Wa pili kutoka kushoto Kaimu Mwenezi CCM Mkoa wa Kagera Hamimu Mahamudu