November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mamlaka Dawa za Kulevya yapeleaka wanasaikolojia Hanang

NA Mwandishi wetu,Timesmajira

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini (DCEA), imetoa wataalamu sita wa saikolojia na masuala ya Ustawi wa jamii, ambao wataungana na wataalamu wengine kutoa huduma katika kambi tatu za waathirika wa maafa ya maporomoko ya tope na mawe Hanang mkoani Manyara.

Akipokea wataalam hao, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amesema kutokana na maafa yaliyowapata waathirika hao wa maporomoko na kupoteza ndugu na mali zao na kupata msongo wa mawazo, kunahitaji kuwajenga kisaikolojia, wanatakiwa kupata matumani ya namna ya kuendelea na kurejea katika hali yao ya awali.

Pamoja na hilo Katibu Mkuu huyo amempongeza Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo kwa hatua hiyo.

Amesema, timu hiyo itaungana na wataalam wengine waliopo kwa ajili ya kuendelea kuwasaidia wananchi hao kwa kuwapa huduma ya unasihi (ushauri) pamoja na elimu ya kujikinga na magonjwa ya afya ya akili wanapoendelea kuhudumiwa na Serikali.

“DCEA imetoa Wasaikolojia hawa ambao watajikita kutoa elimu kwa waathirika wa maafa yaliyotokea, hii ni hatua nzuri kwa kuwafikia na kuwashauri pale inapobidi ili kusaidia kutopata msongo wa mawazo na kupambana na changamoto ya afya ya akili,” amesema Dkt. Yonazi.

Afisa Mwandamizi kutoka mamlaka hiyo, Daniel Kasokola, amesema Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo amechukua hatua ya kutuma timu hiyo kama sehemu ya kutekeleza wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwataka watanzania wote kuungana kuwataidia wahanga hao.

Anaamini kuwa, timu hiyo kwa kushirikiana na wataalam wengine itasaidia waathirika wa maafa hayo kurejea katika hali zao za kawaida.

Naye mwanasaikolojia, Deogtarias Ramale kutoa DCEA amesema, huduma watakazozitoa zitawasaidia kuweza kukubaliana na kilichotokea na mazingira ya sasa kutokana na kupoteza ndugu zao, mali na hatimaye kurejea katika shughuli zao za kila siku.