November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia asikia kilio cha wakazi Usimba, apeleka mil 964

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Kaliua

RAIS wa awamu ya 6 Dkt Samia Suluhu Hassan amesikia kilio cha ukosefu wa shule ya msingi kwa wakazi wa Kijiji cha Magele na sekondari ya kata ya Usimba Wilayani Kaliua na kuamua kuwapelekea sh mil 964 kwa ajili ya ujenzi wa shule 2 ya msingi na sekondari.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti wakazi wa Kijiji hicho wamemshukuru Rais Samia kwa kuokoa maisha ya watoto wao waliokuwa wakiteseka kwa kutembea umbali mrefu kufuata shule ya karibu iliyopo wilaya jirani ya Urambo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho Issa Katabhi amesema tangu waanze kuishi kijijini hapo miaka 35 iliyopita hawajawahi kuwa na shule ya msingi hali iliyopelekea watoto wao kutembea umbali wa zaidi ya 20 kwenda na kurudi shule jirani.

Amebainisha kuwa watoto wao wakiwemo wenye mahitaji maalumu walikuwa wanapata òshida sana hali iliyopelekea baadhi yao kuamua kuacha shule huku wengine wakiongopa kuwa wanaenda shule kumbe wanaishia njiani kutokana na uchovu hivyo kushindwa kuendelea na masomo.

‘Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kusikia kilio chetu na kuamua kutujengea shule mpya yenye ubora wa hali ya juu sana,’ amesema.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Jerry Mwaga, Kaimu Afisa Elimu wa msingi John Moto amesema shule hiyo ni mkombozi kwa kuwa itasaidia kupunguza mlundikano wa watoto wanaosoma katika shule mama ya Usimba ambayo ina watoto zaidi ya 1300 na iko umbali mrefu sana kutoka kijijini hapo.

Amebainisha kuwa ujio wa shule hiyo na shule mpya ya sekondari ya kata hiyo iliyogharimu zaidi ya sh mil 600 ambazo zinatarajiwa kuanza mwezi Januari 2024 ni fursa muhimu kwa wakazi wa Kijiji hicho kwani watoto wao wakiwemo wenye ulemavu watapata fursa ya kupata elimu karibu na nyumbani.

Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt Rashid Chuachua amefafanua kuwa ujenzi wa shule hizo unatokana na azma ya dhati ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka watoto wote wakiwemo wenye ulemavu kupata elimu ili kuongeza idadi ya wataalamu katika sekta mbalimbali.

Amemshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kusikia kilio cha wakazi wa Kijiji hicho na kuwajengea shule ya viwango yenye miundombinu yote.

Kaimu Afisa Elimu Sekondari Mwalimu Robert Toy amesema ujenzi wa shule hiyo ya kata umemaliza kilio cha muda mrefu cha watoto kutembea umbali mrefu wa zaidi ya km 10 kwenda shule ya kata jirani ya Kazaroho.