November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Misaada ya Serikali Hanang yamkuna Mbowe

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Hanang

MWENYEKITI wa CHama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa msaada wa ari na mali kwa waathirika wa maporomopo ya tope na mawe wilayani Hanang, mkoani Manyara na ametoa wito kwa wadau wengine kuendelea kutoa misaada pasipo kuchoka kwenye jambo hilo.

Mbowe ametoa kauli hiyo juzi alipofanya ziara ya kuwatembelea majeruhi wa maafa hayo waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara iliyopo Babati Mjini na Hospitali ya Tumaini, Hanang mjini akiwa ameongozana na viongozi wengine wa chama hicho.

Amesema anaelewa kwamba linapotokea jambo kama hilo ni wajibu wa Serikali kweli, lakini ni wajibu wetu kama binadamu kusaidia pale kama Serikali imeshindwa kutoa vya kutosha.

Amefafanua kwamba wametambua kuwa wagonjwa waliokuwa wamepelekwa katika hospita ya Babati ni wale waliokuwa na hali mbaya zaidi na kweli walikuwa na hali mbaya.

“Lakini sisi kwa jicho la binadamu na la mtu wa kawaida ambaye sio daktari, tumeona wanapewa huduma nzuri na huduma ya kuridhisha kwa kweli, na tumeona afya zao zimeimarika na wachache bado wana hali ngumu,” amesema Mbowe na kuongeza;

“Lakini kwa ujumla wake wengi wana hali nzuri madaktari wameweza kuwatibu na tuna imani Mungu atawaponya.”

kwa upande wa Hospitali ya Tumaini, Mbowe alisema waliona waathirika wengi wao wanaendelea vizuri, wanaendelea kupata matibabu.

“Kwa kweli tumefurahishwa na taarifa kwamba madaktari wameletwa kutoka Mkoa wa Arusha, Dodoma, Singida maeneo mengine ya jirani.

Kulikuwa na msukumo wa madaktari na wauguzi ili kufanya huduma kuwa bora zaidi, kwa hilo sisi tunaona ni jambo jema na limesaidia kupunguza ugumu na athari za tatizo hili,” amesema Mbowe.

Aidha, Mbowe amesema walitembelea maeneo yaliyoathirika wameona miundombinu ilivyoumia, namna nyumba za watu zilivyosombwa na mafuriko na wameona tatizo ni kubwa.

Amewaomba Watanzania kwenye hilo, washirikiane, wapeane na kuwaweka wote walioko kwenye huduma kwenye sara na pale pa kuweza kutoa mchango wa chochote kile, basi ifanyike hivyo.

“Sisi tumekuja tumeona na tumesema twende tukajipange na hivyo natoa rai kwa Watanzania wote, kwa wana CHADEMA wote ebu tutoe kila mmoja alichonacho kidogo kwa sababu athari ni kubwa na tatizo hilo halitakwisha kwa siku mbili, linaweza kuchukua mwezi mmoja au miezi kadhaa kwa sababu kifusi, matope yanatolewa, watu wameathirika kwa njia mbalimbali.

Hawa watu watahitaji msaada kwa njia moja au nyingine, msaada wa kibinadamu kwa muda mrefu ujao, Serikali itafanya yake, lakini na sisi kama wananchi wa kawaida tufanye ya kwetu ili kwa pamoja tshikamane katika tatizo hili,” amesema Mbowe.

Mbowe, amewashukuru wote ambao walikuwa wepesi kupeleka mkono wa heri kwa wathirika hao, hivyo anawaomba wale ambao hawajafanya chochote basi wafanye na wale ambao hawana uwezo, ambacho hakiwezi kupimika kwa njia ya mali na fedha, basi wawaweke watu hao kwenye sala, ili Mungu aweze kuwapa ujasiri na subira ya kukabiliana na jambo hilo, kwa uzito kama lilivyo.

Aidha, Mbowe amesema kwa namna wananchi hao walivyokuwa jirani na mikondo ya maji na kuishi mabondeni, ndivyo kwa namna walivyoathirika zaidi.

Amesema na hilo la watu kujenga kwenye mikondo ya maji katika maeneo mabonde limekuwa ni tatizo sugu nchini kwa muda mrefu, aliomba Watanzania na Serikali yasisubiriwe majanga kama hayo yatokee.

“Ajali ni ajali inaweza kutokea ukiwa milimani, lakini mafuriko ni pale unapokuwa mabondeni, kwa hiyo tujaribu kutengeneza Sera na Serikali izisimamia,”amesema na kuongeza;

Serikali inasema hairuhusu watu kukaa mabondeni, lakini inawapelekea barabara, umeme, maji na inawaruhusu wanajenga ni wazi watakaa,” amesema Mbowe na kuongeza;

“Yakija mafuriko tunaanza hadithi mpya, tuangalie ufumbuzi wa muda mrefu tusione hili jambo la kuishi kwenye mabonde ni jambo jema, kwa sababu inaweza kupita miaka 50, lakini yakatokea mafuriko kwenye mazingira ambayo hauwezi kuyategemea, kama hayo ya Hanang.”

Ameomba hilo, liwe suluhisho la muda mrefu, lakini kwa wale waliokwisha athirika Serikali ifanye tathimini ya kutosha na baada ya hapo, itaweza kuwatambua waathirika wote wa tatizo hilo na kuwatafutia maeneo salama kwa ajili ya kuanza makazi yao mapya na kupata msaada wowote wa kibinadamu ili kuwawezesha upya baada hayo yaliyotokea.